********
Wanawake wajasiriamali nchini wametakiwa kuacha kufanya biashara kwa mazoea badala yake kurasimisha biashara zao ili kupata fursa mbalimbali za kibiashara.
Wito huo umetolewa tarehe 22 Juni, 2022 na Afisa Sheria kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bi. Vicensia Fuko wakati akitoa mada kuhusu huduma zinazo tolewa na Wakala katika Mafunzo ya wanawake wajasiriamali kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Visiwani, yanayofanyika katika ukumbi wa JKT Mgulani Temeke, Jijini Dar es Salaam.
Bi. Fuko amesema wanaporasimisha biashara zao inawapa fursa mbalimbali za kibiashara ikiwa ni pamoja na kupata mikopo kutoka taasisi za fedha na kushinda zabuni.
“Nichukue fursa hii kuwahamasisha wanawake wajasiriamali kuhakikisha kuwa mnarasimisha biashara zenu kupitia BRELA na kwa sasa usajili unafanyika kwa njia ya mtandao, hivyo hakuna haja ya kufika katika ofisi za BRELA, ” amefafanua Bi. Fuko.
Katika mafunzo hayo ya siku nne, washiriki watajadili masuala mbalimbali yatakayowawezesha kujikwamua kiuchumi sambamba na kusherehekea maadhimisho ya miaka 25 ya
kuanzishwa kwa Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote, ambao mwanzilishi wake ni Mama Anna Mkapa.