Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke Bi. Esther Mkokota akizungumza na Wananchi wa Kata ya Chamazi jijini Dar es Salaam wakati akitoa elimu kuhusu rushwa
Wananchi wa Kata ya Chamazi jijini Dar es Salaam wakitoa kero na taarifa katika kikao na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke.
………………………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Wananchi wa Manispaa ya Temeke Mkoa wa Dar es Salaam wameipongeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke kwa kuendelea kutoa elimu kuhusu rushwa jambo ambalo litawasaidia kubaini na kutoa taarifa kuhusu vitendo vya rushwa.
Wakizungumza leo tarehe 22/6/2022 jijini Dar es Salaam katika kikao kati ya TAKUKURU Mkoa wa Temeke na Wananchi wa Kata ya Chamazi kilichofanyika katika kata hiyo, wamesema kuwa wanaishukuru takukuru kwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu rushwa kutokana ni msaada mkubwa katika kupambana na vitendo vya rushwa.
Mkazi wa Kata ya Chamazi Bw. Steven Paul, amesema kuwa elimu ya rushwa kwa wananchi ni jambo la muhimu kwa sababu wananchi wengi hawana uelewa mkubwa kuhusu vitendo vya rushwa vinavyofanyika.
“Tunaiomba TAKUKURU kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa wananchi kuanzia ngazi ya mtaa ili kusaidia watu kubaini vitendo vya rushwa na kutoa kutoa taarifa kwa Mamlaka husika” amesema Bw. Paul.
Bw. Paul amesema kuwa baada takukuru kutoa elimu amejua mambo mengi muhimu ikiwemo ufatiliaji wa miradi ya kimaendeleo inayotekelezwa na serikali.
Mjumbe wa serikali za mtaa wa Rufo Kata ya Chamazi Bi. Seben Cosmas, ameiomba takukuru kuendelea kuchukua hatua za kisheria kwa watu wote watakaobainika kuhusika na vitendo vya rushwa.
“Tunaomba pia waendelee kutoa hamasa katika kata ya Chamazi ili tuweze kupata elimu na kumsaidia Rais wetu katika kufanikisha kazi mbalimbali kwa manufaa ya taifa letu” amesema Bi. Cosmas.
Mkazi wa Kata ya Chamazi Bi. Janeth Godfrey ameeleza kuwa baadhi ya viongozi hawafati sheria na kuleta usumbufu katika jamii.
Amesema kuwa ni vizuri kufata kanuni na taratibu ili kufikia malengo tarajiwa na kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.
Afisa wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke Bi. Esther Mkokota, amesema kuwa utoaji wa elimu kwa wananchi sehemu ya majukumu yao ya kuhakikisha wananchi wanakuwa na uelewa mkubwa kuhusu rushwa.
Amesema kuwa kupitia kikoa cha wananchi wameweza kupokea malalamiko ya rushwa pamoja na kutoa ufafanuzi namna ya kutoa taarifa vitendo vya rushwa.
“Malalamiko yote kuhusu rushwa tunayachukua na tunakwenda kuyafanyia uchuguzi ili kubaini ukweli” amesema Bi. Mkokota.