Na Dotto Mwaibale, Singida
MFANYABIASHARA mmoja maarufu wa mjini Singida mkoani hapa anadaiwa kumteka
na kumficha kusikojulikana kwa zaidi ya miaka 10 sasa mtu mmoja aliyekuwa
mfanyakazi wake na haijulikani kama yupo hai au amefariki.
Madai hayo yalitolewa na Omari Rashid juzi mbele ya Mkuu wa Mkoa wa
Singida, Dk.Binilith Mahenge, kwenye mkutano wa kusikiliza kero za wananchi
uliofanyika katika viwanja vya Stendi ya Zamani Manispaa ya Singida.
Rashid ambaye alidai ni mtoto wa mtu huyo aliyetekwa, alieleza kuwa baba
yao hajaonekana tangu mwaka 2010 baada
ya mfanyabiashara huyo kumlaghai na kuchukua hati ya nyumba yao na kisha
kuwafukuza katika nyumba hiyo ambapo sasa wanaishi kwa kutangatanga.
Aliongeza kuwa mfanyabiashara huyo (anamtaja jina) alimrubuni baba yao
kwamba atamlea na familia yake kwa kipindi chote cha maisha yao lakini katika
hali ya kushangaza wamejikuta wakitimuliwa na mfanyabiashara huyo ambaye
amejimilikisha nyumba yao iliyopo eneo la Majengo Manispaa ya Singida.
Rashid alisema kinachowashanga na kujiuliza maswali yasiyo na majibu ni
kwamba baba yao hajaonekana tangu mwaka huo hali inayowafanya waingiwe na hofu
kama yupo hai au amekufa.
“Mheshimiwa RC utatusaidiaje jambo hili ili tupate nyumba yetu na
tujue hatma ya baba yetu alipo,” alisema.
Kufuatia ombi hilo, Mkuu wa Mkoa Singida, Dk.Mahenge alimwagiza Katibu
Tawala wa Wilaya ya Singida ( DAS) na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Lucas Mwakatundu wachukue maelezo ya kina ya mlalamikaji huyo ili serikali
iweze kuyafanyia kazi madai yake.
Aidha, Dk.Mahenge aliwagiza viongozi kuanzia ngazi za wilaya hadi chini
kujenga tabia ya kuitisha mikutano ya wananchi na kusikiliza kero zao.
Alitumia nafasi hiyo kuwaeleza
wananchi mafanikio mbalimbali yaliyofanywa na serikali ya awamu sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mkuu huyo wa mkoa alisema katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais
Samia Suluhu Hassan Mkoa wa Singida umepatiwa Sh.Bilioni 230 kwa ajili ya utekelezaji wa
miradi ya maji, Barabara, Elimu, Umeme na ya Sekta ya Afya.