Balozi wa Kodi ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani Mhe. Subira Mgalu amewahamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa wakati na kuhimiza matumizi sahihi ya mashine za EFD kwa lengo la kuongeza mapato ya Serikali na hatimaye kuleta maendeleo ya taifa.
Akizungumza wakati wa zoezi la kuhamasisha matumizi ya mashine za EFD mkoani Dodoma, balozi huyo wa kodi amesema kwamba, Serikali inategemea kodi kutoka katika vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kodi zinazokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kuwaletea maendeleo wananchi wake.
“Nikiwa balozi wa kodi, nachukua fursa hii kutoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kulipa kodi kwa wakati na kuhakikisha wafanyabiashara wanatoa risiti sahihi kila wanapofanya mauzo na wananchi wanadai risiti kila wakati wanapununua bidhaa ili Serikali iweze kutekeleza jukumu lake la kuwaletea wananchi maendeleo kupitia miradi mbalimbali,” alisema Balozi Subira.
Naye, Meneja Msaidizi wa TRA Mkoa wa Dodoma Bw. Silver Rutagwelera ameeleza kuwa, lengo la zoezi hilo ni kutoa elimu kwa walipakodi ili waweze kutumia mashine za EFD kwa usahihi na kulipa kodi kwa wakati.
“Dhumuni lingine la zoezi hili ni kuwahamasisha walipakodi wetu kulipa kodi ya mapato awamu ya pili. Pia makampuni pamoja na wafanyabiashara binafsi wenye mauzo kuanzia milioni 100 kuwasilisha ritani za mapato za mwaka 2021 kabla ya tarehe 30 Juni, 2022,” alisema Bw. Rutagwelera.
Kwa upande wake mfanyabiashara wa vipodozi wa Barabara ya 10 mkoni hapa Bi. Mwajuma Pius amesema amelipokea vizuri zoezi hilo kwa sababu wanapata fursa ya kukumbushwa wajibu wao wa kutoa risiti na kulipa kodi kwa wakati.
Bw. Laurent Masanja ni Mfanyabiashara mwingine wa Barabara ya 10 mkoani hapa ambaye amesema kuwa ni muhimu wafanyabiashara wakashirikiana kwa pamoja kulipa kodi kwa hiari kwani kodi ndio inayoisaidia Serikali kupeleka huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi.
Zoezi la kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya mashine za EFD linalofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania ni endelevu na linafanyika mikoa yote hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kulipa kodi kwa hiari na wakati.