Na Mwandishi wetu, Mirerani
WANAWAKE wafanyabiashara wa magonga wa madini ya Tanzanite wa mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamefanya harambee na kupata shilingi milioni 4 za ukamilishaji wa mfumo wa gesi wa shule ya sekondari Tanzanite.
Diwani wa kata ya Mirerani, Salome Nelson Mnyawi amesema fedha hizo zitakamilisha mfumo wa gesi wa maabara ya shule ya sekondari Tanzanite.
Salome amesema shughuli ya harambee ndogo ya kuchangia umaliziaji wa maabara hiyo imeongozwa na mfanyabiashara wa magonga Veronica Charles.
Amesema awali, halmashauri ya wilaya hiyo ilitoa shilingi milioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya shule hiyo hivyo kupungua sh4 milioni za ukamilishaji.
“Ninaishukuru halmashauri ya wilaya ya Simanjiro kwa kutupatia shilingi milioni 30 za ujenzi wa maabara hii ambayo wanawake wa magonga wamefanikisha harambee ya ukamilishaji,” amesema Salome.
Amesema anamshukuru Mkuu wa Wilaya hiyo Dk Suleiman Serera, Mkurugenzi mtendaji Samwel Warioba, Mbunge wa Jimbo Christopher Ole Sendeka, Mwenyekiti wa Halmashauri Baraka Kanunga, madiwani na wataalam kwa kufanikisha maabara hiyo.
Amesema baada ya kuona changamoto hiyo aliwashirikisha wanawake hao ambao walitoa kidogo walichonacho kukamilisha maabara hiyo.
“Wanawake ni jeshi kubwa, tumeshirikiana kwa pamoja na kukamilisha mfumo wa gesi wa maabara hiyo ya shule ya sekondari Tanzanite,” amesema Salome.
Mgeni rasmi wa harambee hiyo, Veronica Charles, amesema wanawake wajasiriamali wa magonga wameiitolea kufanya harambee hiyo kwa ajili ya kukamilisha maabara hiyo ya shule ya sekondari Tanzanite.
“Tumeshirikiana na Diwani wetu ambaye tunafanya naye shughuli hizi za madini na maabara hiyo ikishakamilika itakuwa faida ya wanafunzi hao,” amesema Veronica.