Na Alex Sonna -DODOMA.
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Rajabu Mabele amewataka vijana waliohitimu kidato cha sita wanaotakiwa kujiunga na Mafunzo ya Jeshi la Kujenga taifa kwa mujibu wa sheria kwa mwaka 2022 ambao hawajiripoti mpaka sasa waripoti katika makambi ya JKT mara moja.
Akizungumza na Waandishi wa habari Makao Makuu ya JKT Mkoani Dodoma Mkuu wa Tawi la Utawala wa JKT Brigedia Jeneral Hassan Mabena wakati akitoa taarifa kuhusu vijana walioitwa kuhudhuria Mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria kwa mwaka 2022.
Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema pia JKT imetoa nyongeza ya majina ya vijana waliohitimu elimu ya kidato cha Sita mwaka 2022 kujiunga na mafunzo hayo kwa mujibu wa sheria 2022 kuanzia leo June 22, hadi June 25, 2022 .
Amesema vijana wote hao wanatakiwa kuripoti katika makambi ya JKT yaliyo karibu na maeneo wanayoishi isipokuwa kambi ya JKT Makutupora iliopo mkoani Dodoma na ile ya CUJKT iliyopo Kimbiji Dar es Salaam pamoja na Ruvu JKT iliyoko mkoani Pwani ambayo inapokea wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho.
Amesema kambi hiyo ina miundombinu ya kuwahudumia watu wa jamii hiyo.
Brigedia Jenerali Mabena amefafanua zaidi ya kuwa vijana hao wanatakiwa kuanza kuripoti kuanzia leo june 22 na mwisho wa kuripoti ni Juni 25 mwaka huu.
Brigedia Jenerali Mabena amesema orodha ya majina ya vijana walioitwa awamu ya pili ikiwemo vifaa wanavyotakiwa kwenda navyo inapatikana katika tovuti ya JKT, www.jkt.go.tz.
Pamoja na hayo amewakaribisha vijana wote walioitwa kujiunga na vijana wenzao katika kujifunza Uzalendo,Umoja wa Kitaifa,Stadi za Kazi,stadi za Maisha na utayari wa kulijenga na kilitumikia taifa na mafunzo hayo yamekuwa yakiwasaidia vijana.
Aidha Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele amewataka vijana hao kubeba nyaraka ambazo zitawasaidia katika udahili wa vyuo vikuu ili kuepuka usumbufu wa kuvifuata nyumbani wakati mafunzo hayo yakiendelea katika kambi mbalimbali hapa nchini.