Na Shamimu Nyaki – WUSM, Dodoma
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul amesema Serikali inawajali Makocha wazawa ambao wana sifa, na kupitia Mpango Mkakati wa kuendeleza Michezo wa Mwaka 2021 hadi 2031 imeweka kozi na mafunzo mbalimbali kwa ajili ya kuwaongezea ujuzi Makocha hao.
Mhe. Gekul amesema hayo leo Juni 22, 2022 Bungeni Jiji I Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Antipas Zeno (Malinyi) aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kulinda Ajira za Makocha Wazawa na kuwaongezea ujuzi wa kufundisha nje ya Nchi
“Serikali inajali ajira za wazawa na kwa sasa Kozi fupi mbalimbali zinatolewa kupitia Chuo Cha Michezo Malya na Butimba ambapo hadi sasa Vijana 20 wanapatiwa mafunzo hayo na watakapofuzu watapewa fursa” Amesema Mhe. Gekul.
Mhe. Gekul ameongeza kuwa Tanzania ina Makocha 19 ambao wana viwango wa CAF “A” Diploma ambao wanakidhi viwango kufundisha nje ya nchi
Akiendelea kujibu maswali ya wabunge walioliza kuhusu mpango wa kuendeleza Makocha Wanawake akiwemo Mhe.Fatma Taufiq, Mhe. Gekul amesema kwamba Makocha Wanawake wenye sifa wanapewa kipaumbele na wanahamaishwa kujiendeleza kupata Kozi mbalimbali zinazotolewa ili waongeze sifa na kupata madaraja ya juu.
Katika hatua nyingine Mhe.Gekul Amesema kuwa, suala la Makocha waliofuzu Kozi na Mafunzo yaliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) Mwaka 2016 ambao mpaka leo hawajapatiwa vyeti vyao, Amesema kwamba suala hilo linashughulikiwa na litakapokamilika Makocha hao watapatiwa vyeti Vyao.
Aidha, katika Swali lililoulizwa na Mhe. Mohamed Said Issa (Konde) kuhusu Zanzibar Football Federation (ZFA) kupitia TFF kupata faida zinazotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) Mhe. Gekul amesema suala hilo linashughulikiwa na hivi karibuni Mawaziri wanaosimama Michezo Tanzania Bara na Zanzibar watakaa kikao ambacho pamoja na mambo mengine ni kuhakikisha Zanzibar inafaidika na mgao wa FIFA.