Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb).
*************************
Na. Farida Ramadani na Peter Haule, WFM, Dodoma
Serikali imeeleza kuwa kiwango cha ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi kimeendelea kuongezeka kufikia wastani wa asilimia 8.4 katika kipindi cha Julai 2021 hadi Aprili 2022, ikilinganishwa na wastani wa asilimia 4.3 katika kipindi cha Julai 2020 hadi Aprili 2021.
Hayo yameelezwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande, alipojibu swali la Mbunge wa Tumbatu, Mhe. Juma Othman Hija, alietaka kujua ni kwa kiasi gani lengo la kutoa mikopo kwa sekta binafsi ili kutoa fursa za ajira hususan kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati limefikiwa.
Mhe. Chande alisema kuanzia mwezi Desemba 2021, ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi ulikuwa zaidi ya asilimia 10 ambapo mwezi Aprili 2022 ukuaji huu ulifikia asilimia 13.4.
“Ongezeko hilo linatokana na utekelezaji wa Sera ya Fedha ya Mwaka 2021/22 ambayo imeainisha shabaha ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi wa asilimia 10.6 ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo kwa gharama nafuu na kuongeza ukwasi katika uchumi”, alieleza Mhe. Chande.
Alisema kutokana na mwenendo huo ni matarajio kuwa lengo la ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi la asilimia 10.6 kwa mwaka 2021/22 litafikiwa na hivyo kuchangia uwekezaji, uzalishaji na kuongeza ajira nchini.