Diwani wa Kata ya Nianjema iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Mhe.Abdul Pyalla wa Kati kati aliyevaa kofia akizungumza na wananchi wakati wa ziara yake ya kikazi.
Baadhi ya wananchi wa mtaa wa Magomeni na Nianjema wakiwa katika mkutano huo kumsikiliza diwani wa kata ya Nianjema.
……………………………………
Na Victor Masangu,Bagamoyo
Diwani wa Kata ya Nianjema katika kumuunga mkono Rais wa awamu ya sita Samia Suluhu Hassan katika kuleta chachu ya maendeleo kwa wananchi ameamua kufanya ziara ya kikazi kwa kutembelea mtaa kwa mtaa lengo ikiwa ni kusililiza kero na changamoto zinazowakabili wananchi.
Akizungumza na baadhi ya wananchi wa mitaa ya Magomeni A pamoja mtaa wa Nianjema B Diwani huyo Mhe.Abdul Pyalla alisema kwamba ameamua kuwatembelea wananchi ili kuweza kusililiza kero zao mbali mbali na kuweza kuzitatutia ufumbuzi.
Alifafanua kuwa katika ziara hiyo amejipanga vilivyo kutokana na kuambatana na wataalamu mbali mbali kutoka taasisi za serikali pamoja na mashirika ya umma nia na madhumuni ni kupata majibu ya kina kutoka kwa wataalamu husika.
“Ziara yangu hii lengo lake kubwa ni kutembelea mitaa mbali mbali ambayo ipo katika kata yangu ya Nianjema na dhumuni lake kubwa ni kusililiza kero na changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi wangu katika sekta tofauti,”alisema Diwani huyo.
Aidha aliongeza kuwa lengo lake kubwa ni kuhakikisha kwamba anaweka mipango madhubuti kwa kushirikiana na viongozi wenzake pamoja na taasisi za kiserikali kwa kuwaletea huduma mbali mbali za kijamii ikiwemo upatikani wa umeme,maji,afya elimu pamoja na mahitaji mengine.
“Nashukuru pia katika mkutano huu tumeshirikiana kwa ukaribu na taasisi tofauti Kama vile Tanesco,Dawasa,Tarura,TFS,pamoja na wenzetu wa benki ya NMB ambao wameweza kutoa fursa ya utoaji wa elimu mbali mbali na umuhimu wa kujiunga na bima kupitia benki hiyo,”alifafanua Diwani huyo.
Katika hatua nyingine aliahidi kuendelea kushirikiana bega kwa bega na taasisi zote za kiserikali pamoja na mashirika ya umma kwa lengo la kuweza kutatua changamoto za wananchi na kuweka mipango ya pamoja katika kuwaletea maendeleo yenye tija kwa wote.