Home Michezo SPIKA TULIA AZIMWAGIA SIFA BUNGE SC, TASWA SC

SPIKA TULIA AZIMWAGIA SIFA BUNGE SC, TASWA SC

0

Spika wa Bunge la Muungano wa Tanzania, Tulia Ackson akikagua timu ya waandishi wa habari za michezo katika uwanja wa Jamhuri Dodoma.  Kulia ni meneja masoko wa kampuni ya M-Bet Tanzania iliyoidhamini Taswa SC na kushinda kwa  mabao 2-0 katika mchezo huo.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tulia Ackson na Meneja Masoko wa Kampuni ya M-Bet Tanzania, Allen Mushi wakiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa timu ya waandishi wa habari za michezo kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma. Taswa SC ilicheza na Bunge SC na kushinda kwa mabao 2-0

Spika wa Bunge la Muungano wa Tanzania, Tulia Ackson na Salma Kikwete ambaye ni mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete na baadhi ya wachezaji wa Bunge Queens wakiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa Taswa Queens. Timu ya Bunge Queens iliifunga Taswa Queens mabao 15-13 katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma.

*************************

Na Mwandishi wetu

Dodoma. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tulia Ackson amezipongeza timu ya Waandishi wa Habari za Michezo nchini (Taswa SC) na Bunge SC kwa kupromoti michezo kwa kunyesha mfano kwa vitendo kwa kucheza katika mechi mbalimbali.

Spika Ackson alisema hayo wakati wa mechi maalum ya kirafiki kati ya Taswa SC na Bunge SC iliyofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri, Dodoma na Taswa SC kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Alisema kuwa amevutiwa na jinsi Wabunge na waandishi wa habari na Wabunge wakionyesha vipaji vyao katika mpira wa miguu na netiboli, jambo ambalo litawafanya vijana kuiga mfano wao na kupata wachezaji nyota wa timu za Taifa.

“Kw kweli hii imenivutia sana kwani tutawafanya vijana kuiga mfano na kuwa na wachezaji bora, nawatakia kila la kheri katika jambo hili,” alisema Ackson ambaye pia ni mmoja wa wachezaji nyota wa netiboli wa timu ya Bunge Queens.

Mbali ya Ackson, pia Mama Salma Kikwete ni mmoja wa wachezaji nyota wa timu ya Bunge Queens ambayo inajiandaa na michuano ya Bunge la Afrika Mashariki yaliyopangwa kufanyika Juba, Sudan Kusini.

Kwa upande wake, meneja masoko wa kampuni ya michezo ya kubahatisha ya M-Bet Tanzania, Allen Mushi alisema kuwa amefurahishwa na timu zote mbili na kampuni yao ipo tayari kusaidia timu zote katika shughuli mbalimbali za michezo na kijamii.

“M-Bet Tanzania inajisikia faraja zaidi kushirikiana na Taswa SC katika kufanikisha ziara na tukio hili, pia tupo tayari kusaidia timu ya Bunge SC katika masuala mbalimbali,” alisema Mushi.

Naye Mwenyekiti wa  Taswa SC chairman, Majuto Omary aliipongeza timu ya Bunge SC na kampuni ya M-Bet Tanzania kwa kufanikisha lengo lao la kucheza na waheshimiwa Wabunge kwa mara ya pili.

Nahodha wa timu ya Bunge SC, Cosato Chumi alisema kuwa wamepata kipimo kizuri kuelekea michuano ya Afrika Mashariki na kuipongeza Taswa SC kwa mchezo mzuri.

Wakati huo huo, Taswa SC  iliendeleza rekodi yake ya kutofungwa mwaka huu baada ya kuifunga Bunge SC mabao 2-0. Mabao ya Taswa SC yalifungwa na Waziri Idd na Zicco George.

Katika mchezo huo, Taswa SC iliongozwa na mwenyekiti wake, Majuto Omary  huku Bunge SC ikiongozwa na kepteni fundi Cosato Chumi.

Mbali ya Majuto aka Ronaldo wachezaji wengine waliongara katika mechi hiyo ni Wilbert Molandi (nahodha), Edward Mbaga, Salum Jaba, Saidi Seif, Muhidin Sufiani, Hassan Habani na kipa nyota Ismail Shaaban. Katika mchezo wa pili, Taswa SC iliifunga Utumishi Veterans mabao 3-0. Mabao ya Taswa SC yalifungwa na Waziri, Zicco na Mlanzi.

Katika netiboli,  Bunge Queens iliendelea ‘kuinyanyasa’ Taswa Queens baada ya kuichapa kwa mabao 15-13.