******************************
Adeladius Makwega-BUJORA MWANZA
Juni 19, 2022 Umoja wa Watemi wa Usukuma (UWU) walifanya uzinduzi wa Tamasha la Bulabo ambalo linafanyika kwa juma zima hapa BUJORA-MAGU mkoani Mwanza likishirikisha viongozi wa kiserikali, viongozi wa kidini, viongozi wa wa kimila na wananchi wa maeneo jirani na Magu.
Katika uzinduzi wa tamasha hilo viongozi kadhaa walishiriki, binafsi nilivutiwa na ushiriki wa viongozi wawili mmoja wa kiserikali na mwingine wa kidini. Kwa leo msomaji wangu namtilia maanani kiongozi mmoja wa serikali ambaye ni mkuu wa wilaya ya Busega Gabriel Zakaria iliyopo katika mkoa huu wa Mwanza.
Akiwa amevalia kofia na shati za rangi ya khaki, mheshimiwa Gabriel Zakaria alisimama mara baada ya kupewa nafasi na mkuu wa wilaya ya Magu mheshimwa Salum Kali ambaye ndiye mkuu wa wilaya mwenyeji.
Msomaji wangu naomba ufahamu kuwa wilaya, mikoa na nchi zinazoonekana leo ni mipaka ambayo imewekwa baada ya ujuo wa wakoloni au imewekwa na serikali zetu baada ya mkoloni kwa nia ya kurahisisha huduma kufika katika jamii zetu.
Fahamu kuwa Usukuma unaotajwa katika kabila hili unavuka mipaka ya jiografia ya leo, kitendo cha mkuu wa wilaya ya Busega mheshimiwa Gabriel Zakaria kushiriki katika tamasha hilo iwe kwa mwaliko au kujialika mwenyewe ni kutambua jamii yake anayoiongoza na kuheshimu utamaduni wake. kumbuka na rejea mipaka ya leo imewekwa kurahisha huduma za kijamii tu, Usukuma upo Busega, Usukuma upo Magu na kwingineko.
“Kuheshimu utamaduni ni kuheshimu watu, kudharau utamaduni ni kudharau watu wake.”
Aliposimama kiongozi huyu aliwatambua wageni wote kwa kufuata itifaki na bila ya kuwasahau wananchi walioshiriki ufunguzi huo.
“Ng’wadilah, Emiza, Jawiza.”
Alisalimia umati ulioja kwa sauti yake iliyozoeleka kusikika Redioni na kwenye Runinga wakati akiwa Mtangazaji.
Mheshimwa Zakaria alitoa salaam hizo akiwajulia hali wananchi walioshiriki uzinduzi huo. Kwa desturi za Kisukuma wana koo kubwa mbil EMINZA na NSEYA. Kwa hakika maana yake ni kuwa Magu ni eneo leye ukoo mkubwa wa EMINZA na ndiyo maana mheshimiwa huyu alitoa salaam yenye neno hilo.
Alipomaliza salaam mheshimiwa huyu alisema kuwa amefurahishwa sana na Tamasha hili la Bulabo, waswahili wanasema ukiona vyaelea jua vimeundwa, alimshukuru sana mkuu wa wilaya ya Magu mheshimiwa Kali kwa kumualika katika tamasha hilo.
“Hapa tunapofanya maadhimisho ya kila mwaka tujitahidi kuwe kunapendeza zaidi. Kila mwaka jambo hili liwe linafahamika na jamii yetu na hata jamii nje ya mkoa wa Mwanza na za nje ya Tanzania, kwamba Juni 19-25 ya kila mwkaa ni msimu wa Tamasha la Bulabo.”
Hapa wanaweza wakawepo wafanyabiashara wa kila kitu wakinadi bidhaa zao, ziwe za kimila na hata za biashara za vitu vingine kama chakula na vinywaji, kwa kufanya hivyo tamasha hili litakuwa chanzo kikubwa cha mapato.
Hakuishia hapo aliongeza kuwa Mwanza ni lango kuu la kuingia Mbuga ya Serengeti, kama Tamasha la Bulabo likifahamika zaidi basi hata watalii wanaokuja kutalii wakati wa mwezi juni ya kila mwaka watapata wasaa wa kufika hapa na kuona utamaduni wa Msukuma.
Nina hakika Tamasha la Bulabo lijalo kutakuwa na mabanda ya biashara zote.
“Kwa kufanya hivyo tutaongeza kipato kwa wananchi wetu na kwa kufanya hivyo serikali itakuwa imekamilisha dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuongeza kipato kwa wananchi.”
Alimaliza mheshimiwa Gabriel Zakaria huku wananchi wa Magu waliojitokeza kwa wingi na kuujaza uwanja huo wakishagilia sana.
“Jamani twendeni Bulabo.”
Alisema haya akiwaambia kila mmoja alishiriki amualike mwezake kushiriki tamasha lijalo mwakani.
Alipomaliza mheshimiwa huyu aliketi na Tamasha la Bulabo likaendelea kwa ratiba zingine.