****************************
Na Silvia Mchuruza.
Bukoba, Kagera
Kamati ya uchunguzi wa migogoro ya ardhi imewasilisha taarifa ya uchunguzi wa mgogoro wa ardhi katika kijiji cha Ilemela, Kata ya Gwanseli, Wilaya ya Muleba kwa kuwabainisha wanaomiliki ardhi kihalali na wasiomiliki ardhi kihalali hivyo kutakiwa kuyarudisha maeneo waliyonayo kwa Serikali ya Kijiji.
Akizungumza katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhe. Toba Nguvila amewaeleza wananchi wa kijiji hicho kuwa hakuna ardhi ya kijiji itamilikiwa na mtu bila kufuata utaratibu ikiwemo kuitishwa kwa mkutano wa hadhara ili wananchi kuridhia na kama kuna mtu atamiliki ardhi kinyume na utaratibu huo hatua zitachukuliwa dhidi yake ikiwa ni pamoja na kunyanganywa eneo hilo.
“Kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999 maamuzi ya ardhi ya Kijiji ambayo inatakiwa kutumika kwa ajili ya shughuli fulani au kumilikiwa na mtu ni lazima Mkutano wa Kijiji ukae ufanye maamuzi na wanakijiji wasaini na kuwa na muhtasari kwa ajili ya rejea,” ameeleza Mhe. Nguvila
Aidha, amesisitiza kutengenezwa kwa mpango maalumu wa matumizi bora ya ardhi na kusisitiza ushiriki wa wananchi wote katika mpango huo ili wananchi wote waweze kufahamu ni mipango ipi imepangwa kwa ajili ya matumizi bora ya ardhi ya kijiji.
Sambamba na hayo amesema kuwa kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi utakaowekwa na kupitishwa kuwa eneo la njia ya mifugo ni marufuku mtu mwingine kuziba eneo hilo kwa sababu njia za mifugo zinapozibwa ndo chanzo cha migogoro ya wafugaji na wakulima.
Ripoti ya kamati ya uchunguzi iliyosomwa na Mchunguzi wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Muleba, Inspecta Joseph Dishon ameeleza kuwa vyanzo vya migogoro ya ardhi katika Kijiji cha Ilemela vimetokana na kutofuatwa kwa Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 hivyo ili kuondoa changamoto hizo kamati ilipendekeza yafuatayo:-
Serikali ya Kijiji itambue Maeneo yake na kuyawekea ulinzi ili kuepusha kuvamiwa na wananchi wenye uchu wa ardhi bila kufuata utaratibu na Serikali ya Kijiji imeombwa kuunda kamati maalumu ya kubainisha ardhi zilizorudishwa pamoja na ardhi ambazo umiliki wake haukuwa halali ili ziweze kuwekwa vizuri kwenye kumbukumbu ya ardhi ya kijiji pamoja na kuweka mipaka ya kudumu.
Lakini pia kwa waliojimilikisha ardhi kinyume na utaratibu warudishe ardhi hizo kwenye Serikali ya Kijiji na ardhi zitakazorudishwa zitambuliwe na Serikali ya Kijiji ili ziweze kuwekwa kwenye orodha ya ardhi wazi za kijiji.