Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amewataka wanafunzi kujifunza kwa bidi na kuwa wabunifu hasa katika ulimwengu wa sasa unaobadilika kwa kasi ili kuzikabili changamoto zinazoikabili jamii.
Naibu Katibu Mkuu Yakubu amesema hayo Juni 18, 2022 wakati wa mahafali ya kuwaaga wanafunzi wa hatua ya sita ni sawa na darasa saba, hatua ya 11 sawa na kidato cha nne na hatua ya 13 ambayo ni sawa na kidato cha sita ambayo imefanyika katika viwanja vya shule ya Kimataifa ya Fezza jijini Dar es Salaam.
“Kazi nyingi ambazo zitafanywa na wahitimu wetu katika siku zijazo bado hazijavumbuliwa, ni muhimu wanafunzi wa leo kutambua lengo la shule sio tu kupata maarifa juu ya masomo waliyochagua, wanapaswa kujifunza kubadilika, wawe tayari kupata maarifa mapya, kujitolea kwa kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa” amesema Naibu Katibu Mkuu Yakubu.
Wahitimu hao wametakiwa kuamini katika talanta ambazo wamekuza kwa miaka mingi na kuwa na uhakika wa kuendelea kupata ujuzi na ustadi unaohitajika kwa mafanikio katika karne ya 21.
“Huu sio wakati wa kukaa na kupumzika. Lazima uendelee kujitahidi kujipanua hata Zaidi kidogo kidogo kila siku, kila wiki, kila mwezi na kila mwakam, ndiyo sababu tuko hapa leo, sio tu kusherehekea miradi ambayo tayari imekamilika, kazi za nyumbani ambazo tayari zimefanywa na mitihani tayari imechukuliwa; bali kukubali changamoto ya yote yaliyo mbele yako” amesema Bw. Yakubu.
Akitolea mfano kuhusu umuhimu wa elimu na kutoa changamoto kwa wahitimu hao, wazazi na walezi wa wahitimu hao, Bw. Yakubu amesema aliwahi kusoma mahali kwamba tofauti ya wahitimu wa Harvard na wahitimu wengine, wahitimu wengine wanatafuta kazi, na wahitimu wa Harvard wanavumbua kazi.
Aidha, amewapongeza kwa dhati uongozi, walimu na wafadhili wa shule hiyo kwa majitoleo yao katika kusimamia taaluma ipasavyo na kuifanya shule ya FEZA, mahali bora pa mafanikio kwa wanafunzi wanaosoma shuleni hapo.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule hiyo Bw. CaferJafar Baser amewashukuru walimu na wafanyakazi wote wa shule hiyo kwa kujitolea kuwaandaa wanafunzi kitaaluma katika hatua inayoendelea kuwapa moyo na nguvu ya kuendelea kutoa elimu na kuwa miongoni mwa shule zinazofanya vizuri katika mtihani ya kimataifa.
Mkuu huyo amesisitiza kuwa shule hiyo wanaamini vipaji walivyonavyo wanafunzi wao, vikitunzwa na kuongozwa vyema vitawasaidia na kuwapa fursa ya kuwa viongozi wa kesho katika kuleta maendeleo zaidi kwa taifa na watu wake.