Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kipindi cha kuanzia tarehe 17/06/2022 hadi tarehe 19/06/2022 limefanya misako na doria katika maeneo mbalimbali ya mkoa wetu na kupata mafanikio mbalimbali ikiwemo kukamata watuhumiwa wa uvunjaji wa nyumba na kuiba, wizi na kukamata dawa za kulevya kama ifuatavyo:-
KUPATIKANA NA POMBE HARAMU YA MOSHI.
Mnamo tarehe 17.06.2022 majira ya saa 06:45 mchana, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko Kitongoji cha Kiwira Kati, Kijiji cha Mpandapanda, Kata ya Kiwira, Tarafa ya Ukukwe, Wilaya ya Rungwe na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili 1. HAWA KAPANGALA [40] Mkazi wa Kiwira na 2. EMMANUEL EDWIN MWAKAJELA [50] Mkazi wa kiwira wakiwa na Pombe Haramu ya Moshi @ Gongo kiasi cha lita 04. Watuhumiwa ni muuzaji wa Pombe hiyo, watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi wa shauri lao kukamilika.
KUPATIKANA NA POMBE YA MOSHI.
Mnamo tarehe 18.06.2022 majira ya saa 05:00 asubuhi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko kitongoji cha Mshikamano, Kata ya Nsalala, Tarafa ya Usongwe, Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kumkamata YUNICE GEOFREY MWAKIFWAMBA [40] Mkazi wa Mshikamano akiwa na Pombe Haramu ya Moshi lita 15 akiwa amehifadhi katika madumu mawili ya lita 5 na chupa za maji nne zenye ujazo wa lita 1.5 zikiwa na kuzificha uvunguni mwa kitanda. Mtuhumiwa ni muuzaji wa Pombe hiyo, atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi wa shauri lake kukamilika.
KUPATIKANA NA POMBE ZILIZOKATAZWA NCHINI.
Mnamo tarehe 18.06.2022 majira ya saa 11:00 jioni, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko Kasumulu Kitongoji cha Seko, Kijiji na Kata ya Njisi, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kumkamata ISHENGOMA PETER KASWELA [36] Mkazi wa Ndandalo akiwa na pombe kali zilizopigwa marufuku nchini zikitokea nchini jirani ya Malawi ambazo ni:-
- Ice Dry London Gin box 01 na
- Coferhum box 05 ambazo ni sawa na chupa 120.
Mtuhumiwa ni muingizaji wa bidhaa za magendo na muuzaji wa pombe hizo.
KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WA KUVUNJA NYUMBA USIKU NA KUIBA.
Mnamo tarehe 19.06.2022 majira ya saa 05:30 asubuhi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako dhidi ya wahalifu wa kuvunja nyumba nyakati za usiku na mchana na kuiba huko Mtaa Wa Airport ya Zamani uliopo Kata ya Iyela, Jijini Mbeya na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa watatu ambao ni:-
- SIMON BAHATI MBOYA [29] Mkazi wa Iyela – Mbeya mjini
- ALEX GILBERT RASOBA [22] Mkazi wa Iyela – Mbeya mjini na
- FRANK SANDISA MWASHIWAGALE [23] Mkazi wa Mwakibete – Mbeya mjini.
Watuhumiwa hawa walikuwa wakitafutwa kwa makosa ya uvunjaji wa nyumba usiku na kuiba waliyoyafanya katika wilaya ya Kyela na kisha kukimbilia Mbeya mjini kwa ajili ya kuuza mali hizo. Baada ya kufanyiwa upekuzi kwa mujibu wa sheria watuhumiwa hao walikutwa wakiwa na mali ya wizi TV 01 flat screen aina ya hometech inch 43 ambayo imetambuliwa na mhanga.
Watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa ili kupata mtandao wa watu wanaoshirikiana nao kufanya matukio hayo, kubaini wapokeaji wa mali za wizi pamoja na kupata mali nyingine walizoiba.
KUPATIKANA NA BHANGI.
Mnamo tarehe 19.06.2022 majira ya saa 12:00 jioni, tulifanya msako huko maeneo ya Soko Kuu Tukuyu Mjini, Kata ya Kawetele, Tarafa ya Tukuyu Mjini, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kumkamata ISRAEL MWAKAJUMBA [47] Mkazi wa Kijiji cha Itagata akiwa na dawa za kulevya aina ya bhangi yenye uzito wa kilogramu 01. Mtuhumiwa ni muuzaji wa dawa hizo za kulevya, atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi wa shauri lake kukamilika.
KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WA SHAMBULIO LA KUDHURU MWILI, AIBU NA WIZI.
Mnamo tarehe 19.06.2022 majira ya saa 07:00 mchana, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako dhidi ya wahalifu wa matukio ya shambulio la kudhuru mwili, shambulio la aibu na matukio ya wizi huko Kijiji cha Songwe, Kata ya Bonde la Usongwe, Tarafa ya Usongwe, Mkoa wa Mbeya.
Katika msako huo watuhumiwa watatu walikamatwa ambao ni:-
- WILLIAM KATEMWA [32] Mkazi wa Kijiji cha Songwe aliyekuwa akitafutwa kwa kosa la shambulio la kudhuru mwili.
- MSAFIRI MSONI [26] Mkazi wa Kijiji cha Songwe aliyekuwa akitafutwa kwa kosa la wizi
- ISACK MSONI [20] Mkazi wa Kijiji cha Songwe aliyekuwa akitafutwa kwa kosa la shambulio la aibu.
Watuhumiwa watafikishwa Mahakamani upelelezi utakapokamilika.
Imetolewa na,
Kamanda wa Polisi
SACP – Ulrich Matei
MKOA WA MBEYA.