Na Mwandishi wetu, Babati
WANANCHI 3,009 wa Kijiji cha Gidngwar Kata ya Madunga Wilayani Babati Mkoani Manyara, waliokuwa wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji wameondokana na adha hiyo baada ya mwenge wa uhuru kuzindua mradi wa maji.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu Sahili Nyanzabara Geraruma amezindua mradi huo wa maji wa Madunga wenye thamani ya shilingi 190,085,038.66.
Mradi huo ambao umekamilika kwa asilimia 100 unakwenda kuwanufaisha wananchi wapatao hao 3,009 wa kijiji cha Gidng’war waliopo Kata ya Madunga.
Geraruma amezindua mradi huo baada ya kukagua na kuridhika na maendeleo ya ujenzi wake ambao umejengwa kwa fedha za kutoka kwenye mfuko wa maji wa Taifa na programme ya lipa kwa matokeo (P for R).
Hata hivyo, Geraruma ameagiza uongozi wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Babati kuhakikisha wanawaunganishia huduma hiyo wananchi kwa maeneo hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Babati, Lazaro Twange amesema wananchi wa eneo hilo wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha mradi huo.
“Tufikishie salamu zetu za shukurani kwa Rais Samia kwa namna anavyotekeleza miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali za elimu, afya, maji, miundombinu na mengineyo,” amesema Twange.
Mkazi wa eneo hilo Edward Salaho amesema tangu azaliwe miaka 20 iliyopita hajawahi kuona mwenge wa uhuru ila mwaka huu ameona mbio hizo na zimefika na faida ya mradi wa maji.
“Tunawapongeza RUWASA kwa namna walivyofanikisha mradi huu ambao utakuwa na manufaa kwa wananchi,” amesema Salaho.
Ujumbe mahsusi wa mwenge wa uhuru mwaka huu ni “Sensa ni msingi wa mipango ya maendeleo, shiriki kuhesabiwa tuyafikie maendeleo endelevu ya Taifa’.