Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amefanya ziara katika Makao Makuu ya Kampuni ya Equinor ya nchini Norway inayojishughulisha na utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi tarehe 17 juni 2022 jijini Oslo, Norway.
Akizungumza na uongozi wa kampuni hiyo Waziri mulamula amewahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo tayari kushirikiana nao katika uwekezaji wa sekta ya gesi utaofanyika mkoani Mtwara. Hivyo ni wakati sasa mipango ya utekelezaji wa mradi huo ulioingiwa makubaliano ukawekewa mkazo zaidi.
Waziri mulamula amesema kwakuwa mradi huo baada ya kukamilika unategemewa kuwa wa kwanza kwa ukubwa barani Afrika hivyo ni fursa ya ajira kwa watanzania na italeta suluhu ya changamoto za nishati sambamba na kupunguza matatizo yaliyopo sasa.
Hivyo, ametoa rai kwa kampuni ya Equinor kuweka bajeti ya kujenga uwezo kwa watanzania ili waweze kuwa sehemu ya utekelezaji wake kwa kushiriki kazi za kitaalamu zitakazowawezesha kupata uzoefu kwaajili ya miradi mingine kama hiyo
Naye Makamu wa Rais wa Kampuni ya Equinor, Ms. Unni Merethe Skorstad alieleza kuwa kampuni yake mpaka sasa imetoa zaidi ya nafasi 1000 za ufadhili za masomo katika vyuo vikuu vya nchini Tanzania ambavyo ni pamoja na chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu cha Zanzibar na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Baadhi ya wahitimu waliofadhiliwa na kampuni hiyo wameajiriwa na sekta za nishati za nchini Tanzania na Nje ya Nchi ikiwemo Norway na wengine wameajiriwa kufundisha katika vyuo walivyosoma.
Huduma nyingine za kijamii zinazotolewa na Kampuni ya Equinor kwa Tanzania kufuatia kuingiwa makubaliano ya uchimbaji wa gesi mkoani Mtwara ni pamoja na; kujengea uwezo juu ya uelewa wa mradi huu na manufaa yake kwa jamii itakayozunguka mradi na taifa kwa ujumla, kusaidia sekta ya elimu, afya na kuwajengea uwezo wafanyakazi katika sekta ya nishati hususani katika mafuta na gesi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na ujumbe wake wakiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa kampuni ya Equinor alipotembelea Makao Makuu ya kampuni hiyo tarehe 17 Juni 2022 jijini Oslo, Norway.
Makamu wa Rais wa Kampuni ya Equinor, Ms. Unni Merethe Skorstad akiwatambulisha kwa Mhe. Waziri Mulamula vijana wa kitanzania walioajiriwa katika kampuni ya Equinor na katika vyuo vya Norway katika fani ya mafuta na gesi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na uongozi wa kampuni ya Equinor ya nchini Norway.
Makamu wa Rais wa Kampuni ya Equinor, Ms. Unni Merethe Skorstad na Mshauri Maalum wa Mawasiliano wa Kampuni ya Equinor, Bw. Tarjei Skirbekk wakiwa katika mazungumzo na Mhe. Waziri Mulamula.
Uongozi wa Kampuni ya Equinor ukifatilia mazungumzo.
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania ukifuatilia mazungumzo.
Mazungumzo yakiendelea.
Picha ya pamoja Mhe. Waziri Mulamula na watanzania wanaofanya kazi katika kampuni ya Equinor.