****************************
Na. Zillipa Joseph, Katavi.
Mkuu wa wilaya ya Mpanda Jamila Yusuf amewaonya wanaume wenye tabia ya kutelekeza familia zao mara baada ya kuuza mazao kuacha tabia hiyo mara moja kwani ni mojawapo ya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
Jamila ameyasema hayo wakati akizungungumza na wakazi wa kijiji cha Mwamkulu mahali kunakopatikana mchele mwingi kutokana na kilimo cha mpunga kustawi zaidi katika kata hiyo ambapo amewataka wanaume kuacha tabia hiyo mbaya.
‘Wakati wa kulima unaandamana na mama na watoto kwenda shambani, leo hii mmevuna unauza mazao peke yako kwa kisingizio kuwa wewe ni baba halafu unatoroka unakwenda kuzila hizo hela na watu wengine’ alisema.
Mkuu huyo wa wilaya pia ameongeza kuwa hali hiyo imekuwa ikidhoofisha familia nyingi hali inayopelekea utapiamlo kwa watoto wadogo
‘Sasa unadhani itakuwaje unakuta mtoto anashindia kiazi kitamu kimoja siku nzima ukiuliza unajibiwa hali mbaya’ aliongeza
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya ya Mpanda ameongeza kuwa katika kusikiliza kero za wananchi kwa wiki anapokea zaidi ya wanawake wawili wanaolalamikia kutelekezwa na waume zao.
Awali katika sherehe za siku ya mtoto wa Afrika taarifa ilielezwa kuwa utelekezwaji wa watoto unaofanywa na wazazi unapelekea matatizo mbalimbali kama watoto kujiingiza katika tabia hatarishi kama kujiunga na magenge ya wizi, na kujihusisha na masuala ya ngono.
Katika taarifa hiyo iliyoandaliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda na kusomwa na Frank Moses ambaye ni mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi Kashaulili ilieleza pia kuwepo kwa watoto wengi wenye lishe duni kwa sababu ya wazazi kwa makusudi kuziacha familia chini ya uangalizi wa watoto kwa madai ya kwenda kutafuta riziki kwa kipindi kirefu.
Baadhi ya wazazi waliozungumzia suala hilo wamethibitisha kuwepo kwa tabia ya utelekezaji wa familia ambao umegawanyika katika makundi mawili la kwanza wazazi au walezi kuhamia shambani kwa kipindi cha miezi sita au zaidi kwa shughuli za kilimo na kuacha familia ikijilea chini ya uangalizi wa mtoto mkubwa na pili ni mwanaume kuuza mazao na kuikimbia familia mpaka pale atakapoishiwa ndio ataonekana.
‘Sasa unakuta mtoto aliyeachiwa wenzake ana miaka 14 au 16 hali inakuwa ngumu sana pale nyumbani na wakati mwingine wanalazimika kuomba omba kwa majirani vyakula vinapowaishia ndani’ alisema Beatrice Sedoka mkazi wa Mpanda.