***************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
WANANCHI 2,487 wa Kijiji cha Long’oswan Kata ya Terrat, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara na
mifugo 6,216 watanufaika na mradi wa maji baada ya mwenge wa uhuru kuuzindua.
Meneja wa RUWASA wa Wilaya ya Simanjiro, mhandisi Johanes Martin ameyasema hayo wakati mwenge wa uhuru ulipotembelea na kuweka jiwe la msingi mradi huo wa maji.
Mhandisi amesema awali wananchi wa eneo hilo walikuwa wanatembea umbali wa kilomita nane kufuata huduma ya maji ila hivi sasa wanapata maji hayo yaliyopo mita 400 hadi mita 1,000.
“Mradi huu umegharimu kiasi cha shilingi milioni 321.4 ikiwemo shilingi milioni 312 mbazo ni fedha za Serikali na shilingi 8,500,000 mchango wa wananchi,” amesema mhandisi Martin.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Wakili msomi Dkt Suleiman Hassan Serera, amesema wananchi wameishukuru Serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha mradi huo.
“Wananchi wa eneo hili wamefurahishwa na mradi huu hivyo kwa heshima na taadhima wanaomba utembelee na kuuzindua mradi huu ili wafurahie matunda ya Serikali ya awamu ya sita,” amesema Dkt Serera.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa kwa mwaka huu, Sahili Nyanzabara Geraruma amewataka wananchi wa eneo hilo kuutunza mradi huo.
“Lengo la kumtua mama ndoo kichwani litakuwa limetimia kupitia mradi huu ila wananchi mnapaswa kuutunza kwa faida ya kizazi hiki na kijacho,” amesema Geraruma.