Na Mwandishi wetu, Haydom
MBUNGE wa viti maalum Vijana Taifa kupitia Mkoa wa Manyara, Asia Halamga amesema vijana watamlipa Rais Samia Suluhu Hassan mwaka 2025 kwenye uchaguzi mkuu kwa kumpa kura nyingi za ndiyo kutokana na namna anavyowajali vijana.
Asia ameyasema hayo mji mdogo wa Haydom Wilayani Mbulu, wakati mwenge wa uhuru ukipitia na kuona shughuli za mradi wa kiwanda cha kutengeneza chaki.
Amesema kutokana na shughuli za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia, vijana wengi watampa kura za ndiyo kwenye uchaguzi wa mwaka 2025.
“Vijana tuna jambo letu mwaka 2025 kwa kumpa kura nyingi za kutosha Mama Samia ili kumlipa kwa haya maendeleo anayoyafanya na namna vijana anavyotujali,” amesema Asia.
Amesema unaweza kukesha usiku na mchana ili kuyasema mema na mazuri yaliyofanywa na Rais Samia hapa nchini.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka huu, Sahili Nyanzabara Geraruma amempongeza Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Abubakary Kuuli kwa kufanikisha mradi huo wa vijana wa kiwanda cha kutengeneza chaki.
“Vijana wametumia fursa kwa kuchukua mikopo inayotolewa na halmashauri kupitia mikopo ya asilimi 10 ambayo wanawake wanapata asilimia nne, vijana nne na makundi maalum ya walemavu asilimia mbili.
Amesema kupitia fedha za Serikali vijana watajijenga kiuchumi hivyo wajitokeze kukopa na kufanya shughuli za maendeleo na kurejesha mikopo.
Ujumbe mahsusi wa mwenge wa uhuru mwaka 2022 ni sensa ni msingi wa mipango ya maendeleo, shiriki kuhesabiwa, tuyafikie maendeleo ya Taifa’.