Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na baadhi ya walimu wakuu kutoka shule mbalimbali za sekondari kidato cha tano na sita Mkoa wa Dodoma.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Bihawana Liberatus Ntilema akizungumza wakati wa kikao hicho ambapo aliwasisitiza walimu wenzake kutosita kujitolea kwa hali na mali katika kutimiza wajibu wao kwa wanafunzi.
Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Dodoma Sophia Mbeyu akizungumza wakati wa kikao kilichojumuisha walimu wakuu wa shule za sekondari kwa kidato cha tano na sita Mkoa wa Dodoma pamoja na maafisa wa elimu mkoani humo.
Afisa Elimu Sekondari Kongwa DC Bw. Sudi Abdul akizungumza wakati wa kikao kilichojumuisha walimu wakuu wa shule za sekondari kwa kidato cha tano na sita Mkoa wa Dodoma ambapo alihimiza suala la kujitoa kwa walimu ili kuwasaidia wanafunzi kutimiza ndoto zao.
Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Dodoma Justin Machela akisoma mrejesho wa baadhi ya michango iliyopo kwenye shule za sekondari kwa kidato cha tano na sita Mkoa wa Dodoma mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka na walimu wakuu wa mkoa huo (hawapo pichani) wakati wa kikao kilichojumuisha walimu wakuu wa shule za sekondari kwa kidato cha tano na sita Mkoa wa Dodoma pamoja na maafisa wa elimu mkoani humo.
Baadhi ya walimu wakuu kutoka shule mbalimbali za sekondari kwa kidato cha tano na sita Mkoa wa Dodoma wakifatilia hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka (hayupo pichani) wakati wa kikao
……………………………………….
Na Bolgas Odilo-Dodoma.
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amewataka Walimu Wakuu wa shule za Sekondari kidato cha tano na sita Mkoa wa Dodoma kuwapokea wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano kwa mazingira yeyote.
Hayo ameyasema jijini Dodoma wakati akizungumza na walimu wakuu wa shule za Sekondari kwa kidato cha tano na sita Mkoani humo.
Mtaka ameeleza kuwa, hakuna haja ya kutokumpokea mwanafunzi yeyote aliyechaguliwa kujiunga na kidato cha tano katika shule za serikali kwa sababu ya kukosa mchango wa aina yeyote ile.
“Wanafunzi wote ambao wamepangwa kujiunga na kidato cha tano kwa shule zote za Serikali kwa Mkoa wa Dodoma wapokeeni kwenye mazingira yeyote, awe na mchango au la.
“Kwa kumpokea kwako mwanafunzi huyo hakutoathiri chochote kwako wewe kama mwalimu kwasababu, kama mshahara wako utabaki palepale,” amesema Mtaka.
Aidha aliwataka walimu kutoweka michango mingi ambayo siyo ya lazima kwa wanafunzi ambayo inaweza kusababisha mkanganyiko.
“Kama kutakuwa na michango yeyote basi isizidi kiasi cha shilingi laki moja na elfu hamsini (Tsh. 150,000/=) kwa yale mambo ambayo ni muhimu.
“Na wanafunzi wasilazimishwe kununua kitu chochote kwenye maduka ya shule, mpe mwanafunzi mahitaji yanayohitajika aende akanunue mwenyewe.
“Ikitokea mwanafunzi akanunua ‘track suit’ ambayo imepishana kidogo rangi na uliyotaka anunue isiwe kigezo cha kumrudisha nyumbani,” aliongezea Mtaka.
Sanjari na hayo Mtaka aliwataka Maafisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma pamoja na Wilaya, idara zote za elimu na wakuu wa shule kushirikiana katika kuandaa ‘joining instruction’ moja itakayotumika katika shule zote.