Na WyEST,DSM
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema eneo la Sayansi Teknolojia na ubunifu bado linahitaji kupewa msukumo na hivyo linahitaji wadau wengi katika kuendeleza.
Waziri Mkenda amesema hayo Jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa mwaka wa “Tanzania Academy of Science” (TAAS ) na kuzindua kitabu kijulikanacho Pursuing Excellence, Mastery and Success in Professional Career kilichoandikwa na mwandishi Prof. Awadhi Sadiki Mawenya ambae ni mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam na pia mwanachama wa TAAS.
Waziri Mkenda amesema kwa kuwa TAAS pamoja na mambo mengine inalenga kuendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu itakuwa mdau mkubwa kwetu katika eneo hilo akiongeza kuwa Sheria ya elimu ya mwaka 1978 inampa Waziri fursa ya kuunda timu ya ushauri wa mambo mbalimbali na kuiomba Tanzania Academy of Science kuwa timu ya ushauri kwenye eneo la sayansi teknolojia na ubunifu.
“Nimeona Tanzania Academy of Science mna malengo mengi, kwa kuanzia naomba mjikite kwenye sayansi asilia, fani ya udaktari na teknolojia ili muweze kutoa kipaumbele kwenye maeneo hayo, lakini pia niwaombe msisite kutoa ushauri kwenye masuala ya sayansi,” amesema Prof Mkenda.
Ameongeza kuwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi imeandikwa vijana watapelekwa kwenye vyuo bora duniani kusoma kwenye maeneo ya sayansi teknolojia na tiba hivyo ameiomba TAAS kusaidia kwenye eneo hilo la sayansi.
Waziri Mkenda pia aliweka bayana kuhusu watafiti watakaoandika na kuchapisha kazi zao katika majarida ya hadhi ya juu duniani Wizara katika bajeti ya mwaka 2022/23 imetengwa kiasi cha fedha Sh bilioni moja kwa ajili yao.
“Natoa wito kwa vyuo vikuu, wahadhiri waliobobea kwenye sayansi asilia na fani ya udaktari kuandika na kuchapisha katika majarida ya kimataifa ili waweze kupata fedha hizo,” amesema Waziri Mkenda
Kwa upande wake Rais Tanzania Academy of Science (TAAS) Prof. Yunus Mgaya amesema lengo la TAAS ni kuwa kitovu katika ubora wa uendelezaji na matumizi sayansi, teknolojia na ubunifu kwa maendeleo ya kijamii na uchumi.
Prof. Mgaya amesema katika kutekeleza hilo TAAS imeandaa mpango mkakati wa kuifanya sayansi teknolojia na ubunifu kuwa sehemu ya sekta za kijamii uchumi na umma ikiwa ni pamoja na kuimarisha upatikanaji wa ushauri wa kisayansi.