Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama, akizungumza na watumishi wa Watumishi Housing Investiment (WHI) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa nyumba zinazoendelea kujengwa eneo la Kisasa Njedengwa jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Investment, Dkt. Fred Msemwa akimshukuru Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (Wapili kutoka kushoto) kwa kufanya ziara ya kikazi kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa nyumba zilizopo eneo la Kisasa Njedengwa jijini Dodoma.
Baadhi ya watumishi wa Taasisi ya Watumishi Housing Investiment (WHI) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) kabla ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa nyumba zinazoendelea kujengwa eneo la Kisasa Njedengwa jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama (Wapili kutoka kulia) akielekea kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa nyumba zinazoendelea kujengwa na Watumishi Housing Investiment (WHI) wakati wa ziara yake ya kikazi jijini Dodoma. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Investment, Dkt. Fred Msemwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama akiangalia ramani inayoonyesha mradi wa ujenzi wa nyumba eneo la Kisasa Njedengwa zinazojengwa na Watumishi Housing Investiment (WHI) alipofanya ziara yake ya kikazi jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Investment, Dkt. Fred Msemwa (Wa kwanza kulia) mara baada ya kumaliza ziara yake ya kikazi kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa nyumba eneo la Kisasa Njedengwa jijini Dodoma.
Mwonekano wa nyumba zinazoendelea kujengwa na Watumishi Housing Investiment (WHI) eneo la Kisasa Njedengwa jijini Dodoma.
…………………….
Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema Watumishi Housing Investment (WHI) inajenga nyumba bora za gharama nafuu kwa ajili ya kuwakopesha na kuwauzia watumishi wa umma, ikiwa ni utekelezaji wa kipaumbele cha Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan cha kutatua changamoto ya makazi kwa watumishi wa umma nchini.
Mhe. Jenista amesema hayo akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kukakua utekelezaji wa miradi ya nyumba zinazojengwa na Watumishi Housing Investment (WHI) katika eneo la Njedengwa jijini Dodoma.
Waziri Jenista amesema malengo na maono ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kuwa makazi bora kwa watumishi wa umma nchini, yanakuwa ni kipaumbele kimojawapo katika Serikali ya Awamu ya Sita anayoiongoza.
“Bajeti kuu ya Serikali inayojadiliwa hivi sasa inajumuisha bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambayo katika vipaumbele ilivyoviweka ni kuiwezesha Watumishi Housing kupunguza changamoto ya makazi kwa watumishi wa umma wote nchini,” Mhe. Jenista amefafanua.
Mhe. Jenista amesema kuwa, eneo ambalo Watumishi Housing Investment (WHI) inatakiwa kulifanyia kazi katika mwaka wa fedha 2022/2023 ni kuelekea kwenye halmashauri na wilaya mpya ili kuanza ujenzi wa nyumba bora na za gharama nafuu ambazo zitauzwa au kukopeshwa kwa watumishi au halmashauri kwa utaratibu unaotumiwa na WHI lengo likiwa ni kuhakikisha watumishi wa umma nchini wanapata makazi bora.
Akizungumzia ununuzi wa nyumba zilizojengwa eneo la Njedengwa jijini Dodoma, Mhe Jenista amesema ni nyumba bora na jambo la kufurahisha ni kwamba, kwa asilimia zaidi ya 95 zimenunuliwa na watumishi wa umma.
Ameongeza kuwa, nyumba zilizouzwa zipo za madaraja mbalimbali kulingana na uwezo wa watumishi.
“Jambo la msingi ninalopenda kuendelea kuwasisitiza Watumishi Haousing Investment ni kujenga nyumba zenye gharama nafuu ambazo watumishi wa ngazi ya chini wanaweza kumudu na ikiwezekana zijengwe ambazo zitakuwa na bei ya chini zaidi ya milioni 45”, Mhe. Jenista amesisitiza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Investment (WHI) Dkt. Fred Msemwa amesema mradi huo wa nyumba unaotekelezwa na taasisi yake unahusu ujenzi wa nyumba 133 ambapo nyumba 90 zimeshakamilika na walengwa walishahamia na nyingine 43 ujenzi bado unaendelea.
Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Watumishi Housing Investment (WHI) ina lengo la kujenga nyumba bora za gharama nafuu kwa ajili ya kuwauzia watumishi wa umma na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuwawezesha kupata makazi bora yatakayowawezesha kuwa na ari na morali ya kutoa huduma bora kwa wananchi.