Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mizengo Pinda wakiwa na bangi la ujumbe baada ya maandamano.
Baadhi ya Wanafunzi wakifuatilia matukio mbalimbali katika sherehe ya siku ya mtoto wa Afrika
…………………………………………………..
Na. Zillipa Joseph, Katavi
Watoto wawili wakazi wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi wamelawitiwa na mganga wa kienyeji walipoachwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu na wazazi wao huku mganga huyo akiwa amewarubuni wazazi hao wawaache watoto na tiba itafanyika usiku.
Hayo yamebainika wakati Mkuu wa mkoa wa Katavi Bi. Mwanamvua Mrindoko akizungumza na wakazi wa Mirumba katika Halmashauri ya Mpimbwe katika maadhimisho ya sherehe ya mtoto wa Afrika ambapo amewataka wazazi kutokuwa na mazoea ya kuwaacha watoto peke yao.
Amesema katika matukio hayo yaliyotokea kwa nyakati tofauti mganga huyo aliwarubuni wazazi kuwa tiba itapatikana usiku hivyo wawaache watoto mahali hapo kwa matibabu.
Amesema watoto hao wa kiume wenye umri wa miaka sita na nane; walifanyiwa kitendo hicho cha kikatili na mganga huyo kwa makusudi kwa lengo la kutimiza haja zake.
Aidha amewataka wazazi mkoani hapa kujenga tabia ya kuwa karibu na watoto wao kwa lengo la kufahamu mazuri na mabaya wanayopitia watoto ili kubaini kama mtoto amekumbwa na mambo ya ukatili au anaelekea kukumbwa na ukatili na kuweza kuwaepusha na ukatili ambao ungeweza kujitokeza.
Ameongeza kuwa watoto wanahitaji nafasi ya kuzungumza na wazazi wake na hivyo ukali wa kupitiliza sio mzuri kwa malezi ya watoto.
Aidha amekemea mila zilizopitwa na wakati zinazomkataza mtoto kumtazama baba yake hali ambayo kwa kiasi kikubwa inachangia kusababisha unyanyasaji, na hivyo kushindwa kujenga urafiki baina ya mzazi na mtoto.
Mratibu wa Maendeleo ya mtoto mkoani Katavi Wilson Kennedy amesema kwa mwaka 2020/21 mimba za utotoni zilikuwa 1192, matukio ya ubakaji yalikuwa ni 59, utelekezaji wa familia ulikuwa 165, na ndoa za utotoni 45 hali inayothibitisha kuwa unyanyasaji kwa watoto bado ni tatizo kubwa mkoani Katavi.
Mratibu huyo amesema wanaendesha kampeni za utoaji wa taarifa katika serikali za vijiji na mitaa ili kuweza kutokomeza vitendo hivyo huku wakishirikiana na taasisi mbalimbali zisizo za kiserikali.
Grace Julius ni mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Mirumba, alipoulizwa ni mambo gani mtoto anapaswa kuyafanya ili kuepuka vitendo vya kikatili hasa wa ngono alijibu kuwa ni pamoja na kuepuka kupewa zawadi na kuzungumza na watu usiowajua.
Grace aliongeza kuwa hata kutumwa kufuata soda katika maeneo yanauoza vilezi kama baa na vilabuni ni hatari kwa mtoto kwani anaweza kukumbana na warubuni ambao watamharibia maisha, hali iliyopelekea mkuu wa mkoa wa katavi kumpa zawadi ya shilingi elfu tano kwa majibu mazuri.