Kamishna wa Bima Tanzania, Baghayo Saqware akizungumza katika kikao hicho jijini Arusha.
Kaimu mkuu wa chuo cha uhasibu Arusha(IAA)Prof.Epaphra Manamba akizungumza katika kikao hicho jijini Arusha.
…………………………………….
Julieth Laizer,Arusha.
Wadau wa sekta ya bima ,hifadhi ya jamii na watakwimu bima pamoja na wataalamu wa vyuo vya elimu ya juu wamekutana kujadili wazo la kuanzishwa bodi itakayosimamia watalaamu wa bima nchini ili kuweza kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wao.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika katika chuo cha uhasibu Arusha ( IAA) jijini Arusha kikiongozwa na Kamishna wa Bima ,Dk Baghayo Saqware amesema kuwa,lengo la kukutana na wadau hao ni kujadili wazo hilo ni kutaka kuanzishwa kwa bodi hiyo kama zilivyo bodi nyingine katika sekta mbalimbali.
Dk Saqware amesema kuwa,kwa muda mrefu kumekuwa hakuna bodi inayosimamia wataalamu hao jambo ambalo linasababisha wataalamu hao kukosa haki mbalimbali ambazo zinatakiwa kusimamiwa na bodi husika.
Ameongeza kuwa, kwa hapa nchini tayari kuna wataalamu zaidi ya elfu nane ambao wamehitimu katika vyuo mbalimbali na wanatakiwa kuongozwa na bodi hiyo ili kuwatengenezea utaratibu wa kujiendeleza katika taaluma zao kwani kwa Sasa wakitaka kujiendeleza inawalazimu kufanya na bodi ya nje.
Dk Saqware ameongeza kuwa ,sekta ya Bima imekuwa ikikuwa kila mwaka hivyo ili iweze kutekeleza majukumu yake ikiwemo kusimamia maadili katika sekta hiyo ni lazima kuwa na bodi makini itakayoweza kuwasimamia katika kuendeleza sekta ya fedha .
“Tunatarajia baada ya kukaa na kujadili wazo la kutaka kuanzishwa kwa bodi hii maazimio ya kikao hiki yatafika Wizara ya fedha na mipango ili wazo liweze kufikiriwa na hatimaye serikali kuweza kuanzisha bodi hiyo na tunategemea ndani ya mwaka mmoja au mwaka na nusu tutakuwa tumepata bodi yetu tayari.”amesema Dk Saqware.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa chuo Cha uhasibu Arusha (IAA) ,Prof.Epaphra Manamba amesema kuwa,wakiwa kama wadau muhimu ambao wamekuwa wakitoa wataalamu wa kutosha uwepo wa bodi hiyo utasaidia sana katika ukuaji wa taaluma hiyo ya hifadhi ya jamii ,Bima na watakwimu Bima ambayo itasaidia kusimamia shughuli mbalimbali ikiwemo swala la maadili kwa watalaamu hao.
Prof.Manamba amesema kuwa,kitendo cha kukaa pamoja wataalamu hao na kuweza kujadili wazo hilo ni kutaka kuwa na bodi makini ambayo itafuata sheria na taratibu za nchi na hata kuweza kutatua changamoto zinawazowakabili kama ambavyo zinavyofanya bodi zingine .
Naye Mhadhiri wa chuo cha uhasibu Arusha,Dk Mordecai Matto amesema kuwa,kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na bodi hiyo kwani sekta ya Bima nchini ni sekta ndogo ya fedha na ina majukumu makubwa sana katika jamii na serikali , hivyo inahitaji kuwa na bodi makini ambayo itaweza kuisimamia katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku .