Na Dotto Mwaibale, Bagamoyo
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), umetoa fedha za ruzuku ya uzalishaji
kiasi cha Sh.424,596,015.10 kwa walengwa 1,315 katika Wilaya ya Bagamoyo mkoani
Pwani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Shauri Selenda,
alisema hayo leo (16/5/2022) baada ya wafadhili kutoka Benki ya Dunia (WB) na
ubalozi wa Uswis walipotembelea na kukagua miradi inayoendeshwa na wanufaika wa
fedha za ruzuku zilizotolewa na TASAF.
Alisema fedha hizo zimetolewa katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni
mwaka huu ambapo wanufaika ambao wanaendesha miradi ya kilimo,ufugaji na
biashara ndogondogo walipewa fedha kati ya Sh. 100,000 hadi 500,000.
Alisema walengwa 1315 walionufaika na fedha za ruzuku ya uzalishaji ni kati
ya 1,468 waliolengwa na kwamba katika awamu ya kwanza walengwa 1003 walipewa
ruzuku ya jumla ya Sh. 245,061,048.
Naye Afisa Ufuatiliaji wa Miradi TASAF, Janeth Mtelelah alitoa mchanganuo
kuwa wanufaika wa miradi ya kilimo walipewa ruzuku ya asilimia 60 ya kiwango
walichoomba, wanaofanya biashara ndogondogo walipewa asilimia 50 wakati
asilimia 70 ya ruzuku ilitolewa kwa wanufaika wanaofanya miradi ya ufugaji.
Alisema kuwa utaratibu uliotumika kutoa ruzuku hizo ni kwamba kila mnufaika
aliandika andiko lake la mradi na kisha kuomba fedha ambapo alipatiwa kulingana
na vigezo vilivyopo.
Aidha, wafadhili hao kutoka Benki ya Dunia na Ubalozi wa Uswis ambao ni
Michelle Zini, Stanley Magesa na Paulina Mrosso walitembelea vikundi viwili vya
wanufaika katika Kijiji cha Matimbwa ambapo waliridhishwa na jinsi miradi
inavyoendeshwa kwa ufanisi mkubwa.