SAUTI ya Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu imefika serikalini na katika Mwaka wa fedha wa 2022/2023,imeahidi kujenga barabara ya Handeni-Kibirashi-Kibaya-Kwa Mtoro hadi Singida yenye urefu wa kilomita 460 kwa kiwango cha lami.
Kujengwa kwa barabara hiyo kutarahisisha mawasiliano na kufungua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja nan chi kwa ujumla.
Ahadi hiyo imetolewa Juni 14,2022, Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango Dokta Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
“Serikali ya CCM itaweka msisitizo katika ujenzi wa barabara na kufungua fursa za kiuchumi na zile za kuunganisha Tanzania na nchi jirani kwa utaratibu wa EPC + F ikiwemo barabara hiyo ya Handeni hadi Kwa Mtoro Singida,”amesema.
Safari ya Mbunge Mtaturu kuisemea barabara hiyo.
Septemba 12,2019,Mtaturu akiwa na siku 9 tangu aapishwe kwa mara ya kwanza kuwa mbunge wa Jimbo hilo aliuliza swali bungeni kuhusu barabara hiyo.
“Mh Spika barabara hii ni muhimu sana kiuchumi,na kukamilika kwake kwa kiwango cha lami kutachangamsha eneo hilo kibiashara,je ni lini serikali itaanza kujenga barabara hii ili kusaidia wananchi wa Ikungi na Mkoa wa Singida kupata maendeleo,?”alihoji.
Akijibu swali hilo,aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Hayati Elias Kwandikwa alisema usanifu wa barabara hiyo umekamilika na itaanzwa kujengwa hatua kwa hatua ili kuwanufaisha wananchi wa eneo hilo.
Aidha,Mei 17,2021,akichangia bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi,Mtaturu aliiomba serikali kuongeza fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo ambayo umuhimu wake sio kwenye uchumi tu bali pia kwenye suala la ulinzi na usalama kutokana na kupita sambamba na bomba la mafuta linalotoka Tanga kwenda Hoima.
“Tumeangalia kwenye randama nimeona sasa imetengewa kilomita 20 badala ya 50 zilizotajwa mwanzoni,kutokana na bajeti hii ina maana itachukua muda mrefu kujengwa na kukamilika, niiombe serikali iongeze fedha ili kumaliza barabara hii kwa wakati maana imesubiri kwa muda mrefu,”amesema.
Waswahili wanasema mvumilivu hula mbivu,Mtaturu alivumilia tangu 2019 alipoisemea barabara hiyo kwa mara kwanza tangu awe mbunge na hatimaye serikali imesikiliza sauti yake.
Jitihada hizi za serikali ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),ya 2020-2025,iliyoahidi kuielekeza serikali kuendeleza shughuli za ujenzi ifikie malengo yake ya kuwezesha wananchi kuendelea na uzalishaji kwa ajili ya kuongeza kipato chao.