*************************
Na Mwandishi wetu, Hanang’
MBUNGE wa Jimbo la Hanang’ Mkoani Manyara, mhandisi Samwel Hhayuma Xadhay amempongeza Rais Samia Suluhu kwa namna anavyofanikisha maendeleo mbalimbali kwenye Wilaya ya Hanang’.
Mhandisi Hhayuma ameyasema hayo wakati mwenge wa uhuru ukikagua, ukizindua na kutembelea miradi saba ya maendeleo kwenye Wilaya ya Hanang’.
Amesema mwaka 2020 Rais Samia wakati huo akiwa Makamu wa Rais na mgombea mwenza wa Urais alifika Hanang’ kufanya kampeni na kuomba kura akamweleza changamoto mbalimbali zinazowakabili.
“Nilimwambia Mama Samia changamoto zetu za miundombinu ya barabara, maji na miradi mbalimbali ya maendeleo na sasa anaifanyia kazi na tunaona,” amesema mhandisi Hhayuma.
Amesema kwenye suala maji na nishati ya umeme Wilayani Hanang’ Rais Samia ametoa fedha nyingi kufanikisha miradi hiyo na vituo vya afya na zahanati zinajengwa maeneo mbalimbali Hanang’.
Hata hivyo, amewataka wananchi kulipa kodi kwani mwisho wa siku ndizo ambazo zinafanikisha maendeleo yanayoonekana.
“Hata haya madarasa mawili ya shule ya sekondari Ganana, fedha zake zimetokana na tozo za miamala ya simu na fedha za Serikali kuu,” amesema mhandisi Hhayuma.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka huu, Sahili Nyanzabara Geraruma amesema Rais Samia Suluhu Hassan amefaniiisha miradi mingi ya maendeleo nchini.
“Endapo tukiamua kukagua miradi ya maendeleo ya kila Wilaya iliyofanikishwa na Rais Samia tungekuwa tunakesha kwa namna ilivyomingi na yenye tija,” amesema Geraruma.
Mkuu wa Wilaya ya Hanang’ Janeth Mayanja amesema mwenge utaona mradi endelevu wa maji wa Gidangu na kuzindua madarasa manne ya shule ya sekondari Nangwa.
Amesema pia mwenge utaweka jiwe la msingi jengo la dharura hospitali ya Wilaya ya Tumaini na kutoa hundi kwenye mradi wa maendeleo.
“Mwenge utatembelea klabu ya wapinga rushwa, kutembelea na kuona barabara ya kiwango cha lami ya Mkapa na kuzindua kikundi cha vijana Drem studio & stationary,” amesema Mayanja.
Ujumbe mahsusi wa mwenge wa uhuru mwaka 2022 ni sensa ni msingi wa mipango ya maendeleo, shiriki kuhesabiwa, tuyafikie maendeleo ya Taifa’.