***************************
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imewataka wabunifu kusajili Bunifu zao BRELA ili kuona matunda ya kazi zao.
Akizungumza katika Warsha ya Miliki Ubunifu katika chuo Chuo Cha Don Bosco jijini Arusha leo tarehe 16 Juni, 2022, Afisa Sheria kutoka Idara ya Miliki Ubunifu Bw. George Msaki amesema imefika wakati kila mbunifu aone matunda ya anacho kifanya kwa kujisajili BRELA.
Amesema ana imani kuwa elimu ya Miliki Ubunifu wanayoitoa vyuoni italeta chachu kwa watalam kuendelea kuvumbua na kumiliki kisheria bunifu zao kwa ajili ya maendeleo binafsi na Taifa kwa ujumla.
“Vumbuzi nyingi zipo vyuoni ndiyo maana tukaanzia huku kutoa elimu hii, tunaamini mmeelewa na matokeo yataonekana kupitia ongezeko la usajili,” amesema Bw.Msaki
Amewasihi pia wanafunzi hao kurasimisha biashara zao kupitia Mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao unaojulikana kama ORS.
Bw. Msaki amesema zoezi la utoaji elimu ya Miliki Ubunifu ni endelevu na litafanyika nchi nzima.