TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MAONI YA WADAU JUU YA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA
2022/2023
15 JUNE 2022.
Bajeti yenye Mrengo wa Kijinsia: Chachu ya uchumi ya Kiuchumi na Maendeleo Jumuishi
ya Watu.
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na wadau kutoka Mtandao wa Bajeti yenye
Mrengo wa Jinsia ambao ni zaidi ya Asasi za Kiraia 100 na wanajamii kutoka mikoa mbalimbali
tulipata fursa mnamo tarehe 14 Juni 2022 kupitia Mjadala wa Bajeti kufuatilia kwa pamoja na
kuchambua bajeti ya taifa ya mwaka wa fedha 2022/23 iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa
Fedha na Mipango, Mhe. Mwingulu Lameck Nchemba, na baadae kutoa maoni yetu ya bajeti hiyo
iliyotanguliwa na hali halisi ya uchumi wa Tanzania.
Kama inavyojulikana bajeti kuu ya Taifa inatoa mwelekeo wa mipango ya maendeleo kwa kila
sekta kwa mwaka husika.
Hii huonesha ni kwa namna gani serikali imejipanga na kupendekeza
mwelekeo wa namna afua zilizopendekezwa katika sekta mbalimbali zitagharamiwa ili kuleta
mabadiliko, kwa kuwaletea wananchi wake maendeleo kulingana na mahitaji yao au malengo ya
Taifa.
Bajeti hii ya mwaka wa Fedha 2022/23 ni bajeti ya pili katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa
Maendeleo wa Taifa (FYDPIII) na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria kutoa kipaumbele
katika masuala ya usawa wa kijinsia.
Tunaipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kwa nia yake
ya kuendelea kusimamia sera na mipango ya maendeleo kwa manufaa ya Taifa na watanzania kwa
ujumla.
Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 tumeshuhudia kuwepo kwa jitihada za kuboresha
masuala ya kijinsia katika sekta mbalimbali, ambazo kwa kiwango kikubwa zinawagusa
wanawake, vijana na makundi mengine yaliyoko pembezoni, hata hivyo, bado kuna maeneo
yanayohitaji kufanyiwa kazi zaidi ili bajeti iwe na mrengo wa kijinsia na iwe chachu ya uchumi
jumuishi kwa maendeleo ya watu.
Pamoja na mambo mengi ambayo yapo kwenye bajeti ya Mwaka huu, yapo masuala yakupongeza
ambayo ni pamoja na:
Dhamira ya Serikali kuweka mikakati ya kupunguza gharama za uendeshaji kwa kupunguza
gharama za ununuzi wa magari, vipuri na mafuta kwa kuwakopesha watumishi wa umma
wanaostahili kuwa na magari na hivyo kupunguza gharama kutoka bilioni 558 hadi bilioni 50;
kuboresha michakato ya manunuzi kwa kuzingatia gharama zilizoko sokoni badala ya bei ya
mzabuni na kuhamasisha matumizi ya TEHAMA ikiwemo kufanya mikutano ya mitandaoni ili
kupunguza gharama za kujikimu, usafiri na muda unaotumika kushiriki mikutano mbalimbali.
Tunatarajia hatua hizi zitasaidia Serikali kupata fedha za ziada zitakazoelekezwa kuboresha
huduma za kijamii ikiwemo kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto na hivyo, kupunguza
vifo vya kina mama na watoto chini ya miaka mitano; kuboresha mazingira ya elimu ili kusaidia
mazingira bora kwa watoto wa kike na wenye ulemavu kuweza kusoma bila changamoto.
Tunatoa wito kwa serikali kufanya uchambuzi yakinifu wa kijinsia ili kuhakikisha kuwa fedha
hizo zitakazopatikana baada ya kubana matumizi zinatumika vizuri ili makundi ambayo
yanachangamoto zaidi za kijinsia yaweze kusaidiwa.
Sambamba na hilo, Serikali imedhamiria kutatua changamoto za rushwa hasa wakati wa makadirio
ya kodi ambapo maafisa wasiokuwa waaminifu wanakadiria kodi kubwa ili waweze kutengeneza
mazingira ya rushwa.
Kwa kufanya hivi serikali inapoteza mapato ambayo yangesaidia kuboresha
huduma za jamii. Serikali imependekeza marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato ili kuweka
kiwango cha asilimia 3.5 kwa walipakodi wenye mauzo ya kati ya Shilingi milioni 11-100 kwa
mwaka kwa lengo la kuweka uwazi na kurahisisha makadirio na ulipaji wa kodi, hivyo kudhibiti
udanganyifu huo.
Kwa upande Serikali imepunguza tozo kwenye mashine ya EFD ili kuhamasisha
wafanyabiasha kuwa na EFD mashine na hivyo kuongeza upatikanaji wa kodi kwa Serikali.
Ikiwa mkakati huu utatekelezeka na kuweza kupunguza rushwa, tunarajia kuwa kodi hizo
zitakazopatikana kwa wingi zitapelekwa kuboresha huduma za kijamii, ikiwemo afya hususan
bima ya afya kwa wote, elimu na maji, hususani maeneo ya vijijini ambapo bado wanawake,
watoto wakike, na makundi mengine yaliyopembezoni yana changamoto kubwa ya huduma hizo
na hivyo, kupelekea maendeleo duni ya watu katika maeneo hayo.
Tunatoa wito kwa serikali kuendelea kutoa elimu ya umuhimu wa kulipa kodi na kuendelea
kuwawajibisha maafisa wasio waadilifu wanaotumia kodi za wananchi kwa manufaa yao binafsi,
na kubwa zaidi, kuhakikisha kuwa kodi zinazotolewa na wananchi zinaenda kuboresha maisha
yao.
Tumeshuhudia ongezeko la bajeti ya Wizara ya Kilimo kilimo kutoka Bilioni 294 hadi Bilioni 954.
Hii inaonesha dhamira na nia ya dhati ya Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mh. Samia
Suhulu Hassani, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuleta mageuzi katika sekta ya
Kilimo. Bajeti hii ya kilimo pia imelenga kuongeza ajira 3,000 kwa vijana, tunategemea kwa hali
hii changamoto za ajira kwa vijana zitapata ufumbuzi kwa kiwango fulani.
Tunatoa wito kwa
Serikali kuhakikisha kuwa vijana wote wa kike, wa kiume na wenye mahitaji maalumu
wananufaika na ajira hizi zitokanazo na kilimo. Ikumbukwe kuwa kilimo kinaajiri takribani
asilimia 58.1 ya watanzania, ambapo zaidi ya asilimia 80 ni wanawake.
Hivyo, ni muhimu sana
vijana wa kike nao wanufaike na bajeti hii.
Waziri wa kilimo katika hotuba yake alisema kuwa
atapitia mfumo wa ukobeshaji ili kuwawezesha wakulima wasio na dhamana ya kukopeshwa,
wengi wao wakiwa ni wanawake na vijana.
Kwa upande mwingine, Rais Samia katika hotuba yake
ya kwanza Bungeni alisema kuwa ataleta mapinduzi kwenye kilimo na kuhakikisha kuwa
wanawake wananufaika na kilimo.
Tunatarajia kauli ya Mhe Rais, sasa itatekelezwa kwa vitendo.
Kwa upande wa Elimu, kufutwa kwa ada ya kidato cha tano na sita ni jambo la kupongeza kwa
imani kuwa hatua hii itawapa fursa watoto wa kike kuepuka ndoa za utotoni hasa zile zinazotokana
na kisingizio kuwa mzazi hana uwezo wa kumsomesha zaidi.
Licha ya hatua hii nzuri, tutoa wito
kwa Serikali kuzingatia uboreshwaji wa miundo mbinu na mazingira rafiki yatakayowawezesha
watoto wa kike na wale wenye ulemavu kusoma bila changamoto.
Tunapenda kuikumbusha
Serikali juu ya utengwaji wa bajeti kuweza kuboresha miundo mbinu na mazingira ya
kuwahamasisha wanafunzi walioacha masomo kwa sababu mbalimbali kurudi shule.
Watoto
wanaomaliza kidato chan ne ni wengi, hivyo tunatarajia fursa hii ya elimu bila dada itakwenda
sambamba na kuongeza shule na walimu zaidi ili wanafunzi wanaomaliza kidato chan ne waweze
kwenda moja kwa moja kidato cha sita hususan wasichana ambao wamekuwa wakiikosa fursa
hiyo ya elimu kwa muda mrefu.
Katika sekta ya Madini, tunapongeza Serikali kwa kutafuta fursa za kutoa mikopo kwa wachimbaji
wadogo.
Hili ni jambo jema sana ila tunatoa wito kwa Serikali kufanya uchambuzi yakinifu wa
kijinsia ili kuhakikisha kuwa wachimbaji wadogo wadogo wanawake, vijana na makundi mengine
wananufaika na mikopo hiyo.
Lakini pia kuhakikisha kuwa mikopo hiyo inakuwa na masharti
nafuu ambayo makundi hayo wataweza kuyamudu.
Tunaipongeza pia Serikali kwa dhamira yake ya kuwasaidia wamachinga. Hata hivyo
tumesikitishwa na kitendo cha kupunguza asilimia 10 %ya Halmashauri ambayo ilikuwa ni kwa
ajili ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Ikumbukwe kuwa asilimia 10% ya mikopo
isiyo na riba ya Halmashauri ilikuwa msaada mkubwa kwa wanawake na ilikuwa bado haitoshelezi
mahitaji. Hata kama kulikuwa na mapungufu ingekuwa vizuri kushughulikia mapungufu hayo.
Tunashauri asilimia 5% za kusaidia wamachinga zitafutiwe chanzo kingine cha mapato na si
kutumia fungu hilo la wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Kwa kuondoa asilima 5%
inaonesha kwamba tunarudisha nyuma juhudi za kuwakomboa kiuchumi wanawake, vijana na
watu wenye ulemavu kiuchumi.
Ni mategemeo yetu kuwa Serikali itaendelea kuimarisha uwezeshaji wa wanawake kiuchumi
kupitia programu ya kizazi chenye usawa (Generation Equality Forum) ambapo Raisi wetu Mhe.
Samia Suluhu Hassan ni kinara katika afua ya uwezeshaji wa wanawake kiuchumi. Tulitegemea
kuwa hizi asilimia 10% zitaongezeka katika bajeti hii si kupunguzwa. Hivyo tunaiomba Serikali
kutafuta eneo lingine la kupata asiliam 5% kwa ajili ya wamachinga.
Pia, tunashauri Serikali
kuhakikisha kuwa wanawake wamachinga pia wananufaika na mikakati inayoendelea ya
kuwainua wamachinga kwa kuwa kwa asilimia kubwa viongozi wa majukwaa ya wamachinga ni
wanaume hivyo kuna hatari wanawake wakaachwa nyuma.
Tunatarajia Waziri wetu Mwigulu
Lameck atarudisha ile asilimia 10% ya Wanawake, vijana na Watu wenye Ulemavu na Kutafuta
chanzo kingine cha 5% kwa ajili ya Wamachinga.
Mwisho, tunashauri kiasi cha fedha ambacho kinawekwa kwenye mipango, na kupitishwa Serikali
ihakikishe kinatolewa na kutumika ipasavyo ili kuleta tija kwa jamii lengwa.
Tamko hili limetolewa na
Lilian Liundi
Kwa niaba ya wadau walioshiriki mjadala wa bajeti ya taifa 2022/23.