Mkuu wa mkoa wa
Iringa Queen Sendiga akiongea na wadau wa umeme pamoja na wafanyakazi wa shirika la TANESCO mkoa wa Iringa wakati wa uzinduzi wa mfumo wa Nikonekt
Mkuu wa mkoa wa
Iringa Queen Sendiga akishuhudia namna gani ambavyo mfumo wa Nikonekt unavyofanya kazi wakati wa uzinduzi wa mfumo wa Nikonekt mkoa wa Iringa.
Na Fredy Mgunda,Iringa.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)
Mkoa wa Iringa limezindua rasmi Mfumo rahisi wa maombi ya huduma ya Umeme kwa
njia ya Mtandao ‘Kidigitali’ maarufu NI- KONEKT huku likiwaomba wananchi
kuchangamkia fursa hiyo ambayo inamrahisishia mteja kupata huduma za umeme bila
kufika katika ofisi za TANESCO.
Uzinduzi huo umefanyika katika ofisi
za TANESCO Mkoa wa Iringa na kuhudhuriwa pia na wateja wa TANESCO waliofika
kupata huduma za umeme.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa
Mfumo wa Ni – Konekt, Meneja wa TANESCO nyanda za juu kusini Mhandisi Satco
Nombo alisema Mfumo wa Ni- Konekt unamuwezesha mteja kutuma na kufuatilia
maombi ya umeme kwa njia ya kidigitali, kutoa taarifa za dharura, kufanya maombi
yasiyo ya umeme kutoa malalamiko pamoja na kufanya maulizo mbalimbali.
“Kupitia mfumo huu wateja wetu
watapata huduma ya umeme kwa urahisi na haraka huko waliko wakiwa wanaendelea
na shughuli zao, kila kitu kitafanyika kwa njia ya digitali. Huduma hii inarahisisha
sana kwa wafanyabiashara wanaohitaji huduma zetu. Pia itapunguza manung’uniko
mbalimbali na mianya ya rushwa na vishoka..Ukiomba maombi SMS itakuja, hatua
tutakazokuwa tunazifanya SMS itakuja kwa hiyo utakuwa unajua kila hatua
inayoendelea”,alisema.
Mhandisi Nombo amesema ili
mteja/mwombaji aweze kupata huduma ya maombi ya umeme kupitia mfumo wa Ni-
konekt anapaswa kuwa na kitambulisho cha Taifa (NIDA) huku akieleza kuwa Mfumo
huo unatumia njia kuu tatu kufanya kazi yaani maombi kupitia Kiswaswadu (USSD
Code), Tovuti (Web portal) na Programu tumishi (Nikonekt Mobile App).
Ameeleza kuwa mteja anaweza kutumia
mfumo wa Nikonekt kwa kutumia njia ya Tovuti (Web portal) ya www.tanesco.co.tz ambapo
mteja anaweza kutumia simu janja, komputa au kifaa kingine chenye uweo wa
Intaneti.
“Njia zinazotumika kupata mfumo wa
Ni- konekt ni pamoja na kutumia namba maalumu za USSD Code (Kiswaswadu) kwa
kupiga namba *152*00# kwa watumiaji wa simu za kawaida. Bonyeza *152*00#, nenda
namba 4 (Nishati) kisha nenda tena namba 4 (TANESCO) baada ya hapo nenda namba
1 (Maombi ya umeme) baada ya hapo utaulizwa unahitaji kwa matumizi ya
nyumbani/biashara/taasisi…Kila hatua unayofanya utakuwa unapatiwa Ujumbe (SMS)
kwenye simu yako”,amesema Mhandisi Mangara.
Amesema njia nyingine ya kutumia
mfumo wa Ni- konekt ni kupitia Ni-konekt Mobile App ambapo
mteja anaweza kupakua Programu ya Ni- konekt kwenye simu yenye uwezo wa
Intaneti ambapo App ya Ni-Konekt inapatikana kwa watumiaji wote wa simu janja
(Smartphone). Kwa watumiaji wa Android, Aplikesheni ya Nikonekt inapatikana
kwenye Play store na App store kwa watumiaji wa Iphone.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa
Iringa Queen Sendiga alisema kuwa analipongeza shirika la umeme Tanzania (TANESCO)
kwa kazi nzuri wanayoifanya kutoa huduma ya umeme kwa wananchi.
Sendiga alisema kuwa uwepo wa umeme
unasaidia kuchochea maendeleo kwa wananchi kwa kurahisisha shughuli mbalimbali
ambazo mara nyingi zinahitaji nishati hiyo.
Alisema kuwa kuanzia mfumo wa
Nikonekt utasaidia wananchi kupata huduma kwa haraka bila kutapeliwa na vishoka
ambao awali walikuwa wanawatapeli wateja wa TANESCO.
Sendiga alisema kuwa mfumo huo mpya
unaendana na mabadiliko ya teknolojia ya sasa hivyo wateja ambao wanahitaji
kuunganishiwa umeme wanaweza kutuma maombi wakiwa nyumbani na kuokoa muda wa
kwenda kwenye ofisi za shirika hilo.
Alimalizia kwa kusema kuwa mfumo huo
unapunguza gharama za wananchi kutoka eneo moja kwenda ofisi za tanesco kwa
ajili kuunganishwa umeme.
Nao baadhi ya wananchi wameipongeza
TANESCO kuanzisha mfumo wa Ni – Konekt ambao amesema utawapunguzia wananchi
muda na gharama za kufuata huduma za umeme katika ofisi za TANESCO