Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Doroth Gwajima, akizungumza leo Juni 15/2022 wakati wa maadhimisho ya kupinga ukatili kwa wazee yaliyofanyika kitaifa katika Kijiji cha Kisharita Wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis, akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Katibu Mkuu Wizara wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Zainabu Chaula akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Taifa, Lameck Sendo, akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Doroth Gwajima, akisalimiana na Wazee mara baada ya kuwasili kwenye maadhimisho hayo.
Wananchi wa Kijiji cha Kisharita wakiserebuka katika sherehe hiyo.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kisharita wakiwa kwenye maadhimisho hayo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Iramba, Pius Sangoma akizugumza kwenye maadhimisho hayo.
Mwenyekiti wa Machifu Mkoa wa Singida, Mugheni Sengi akizungumza kwenye maadhimisho hayo. |
Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Doroth Gwajima, akitoa kwa Neema Msengi ambaye ni mmoja wa ndugu wa Wazee watatu waliouawa kikatili katika Kijiji cha Kisharita Wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye maadhimisho hayo. |
Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Doroth Gwajima, akizungumza na vijana wa SMAUJATA. |
Afisa Mradi wa Sight Savers, Mradi wa Boresha Maisha, Edwin Barongo akizungumzia kuhusu shughuli mbalimbali zikiwemo za kuwapa huduma wazee. |
Programu Meneja wa Shirika la HelpAge Tanzania, Joseph Mbasha, akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Shabani Muhali kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri wa Wazee Manispaa ya Singida, Juma Mudida, alihoji kwanini watuhumiwa wa mauaji ya wazee wa Kijiji cha Kisharita hawajapatikana hadi leo.
Wazee wakiwa katika maadhimisho hayo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Iramba, Pius Sangoma akiserebuka na Wanafunzi wa Shule ya Msingi, Kisharita.
Mwenyekiti wa Machifu Mkoa wa Singida Chifu Mughenyi Sengi (kushoto) na Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Manispaa ya Singida, Juma Mudida wakiserebuka na wanafunzi wa Shule ya Msingi Kishirita.
Wananchi wa Kijiji cha Kishirita wakiwa kwenye maadhimisho hayo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iramba, Ashery Samwel aakizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Doroth Gwajima, akizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Msingi, Kisharita.
Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Iramba, akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Innocent Msengi akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Doroth Gwajima, akizungumza na mtoto Anna Hatibu baada ya kuhutubia katika maadhimisho hayo.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iramba, Ephrahim Kolimba (kushoto) akiwa kwenye maadhimisho hayo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
SERIKALI imewapatia vitambulisho vya bima za afya vya msamaha wa matibabu wazee 937,266 ambao ni kati ya 1,547,038 waliotambuliwa katika mikoa 26 hapa nchini.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Doroth Gwajima, alisema hayo Leo 15/6/2022 wakati wa maadhimisho ya kupinga ukatili kwa wazee yaliyofanyika kitaifa katika kijiji cha Kisharika Wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Alisema serikali imewapatia vitambulisho hivyo wazee ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kimaendeleo na za kijamii kutokana na kutambua na kuthamini mchango wa wazee pamoja na kuhakikisha maswala mazima ya ulinzi na usalama kwa wazee.
Dk.Gwajima alisema Serikali ilianzisha Kampeni ya MZEE KWANZA yenye lengo la kumpa kipaumbele mzee katika maeneo yote ya kutoa huduma ambayo inalenga kuelimisha jamii kutambua na kuheshimu mchango wa wazee na wakati huo ikikumbusha kuwa kila mmoja ataupitia uzee.
Kuhusu suala la ukatili dhidi ya wazee, alisema katika juhudi za kupambana na ukatili kwa wazee Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawane na Watoto (MTAKUWWA) wa mwaka 2017/18-2021/22 na Mkakati wa Kitaifa wa kutokomeza Mauaji Dhidi ya Wazee 2018/19-2022/23.
Alisema kwa takwimu zilizopo katika Jeshi la Polisi kwa mwaka 2021 nchi imekuwa salama kwani hakuna mzee aliyepoteza maisha kwa njia ya mauaji.
Hata hivyo, Dk.Gwajima alisema kwa mwaka 2022 mwanzoni, nchi iliingia katika dosari kubwa kutokana na mauaji ya wazee yaliyotokea katika mikoa mbalimbali kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kiuchumi na Imani za kishirikina.
“Hapa mkoani Singida Wilaya ya Iramba katika Kijiji hiki cha Kisharika tulipoteza wazee wetu watatu kwa siku moja na wote wakiwa ni wanawake, niombe vyombo vya usalama na wananchi wote kwa ujumla kuhakikisha kuwa kila mtu anatimiza wajibu wake kuhakikisha wote tunakuwa salama na matukio haya kutojirudia tena,” alisema.
Dk.Gwajima alitumia fursa hiyo kuziagiza halmashauri zote nchini kuitumia Kampeni ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii (SMAUJATA) ili isaidie kutokomeza vitendo vya ukatili kwenye halmashauri.
Kuhusu matunzo kwa wazee wasio na uwezo, alisema Serikali imeendelea kutoa huduma ya matunzo kwa wazee kwenye makazi 14 yenye jumla ya wazee 271 wanaume wakiwa 161 na wanawake 110.
Aidha, Dk.Gwajima alisema Serikali ina mpango wa kuanzisha makazi ya wazee kikanda na kutoa elimu kwa jamii ili familia ziweze kuwalea wazee wao na wale wachache watakaokosa huduma katika familia kupata matunzo katika makazi hayo yatakayoanzishwa.
“Vilevile serikali iko katika mchakato wa kuanzisha miradi katika makazi ya wazee ili makazi hayo yaweze kujiendesha na kupunguza utegemezi kwa serikali,” alisema.
Aliongeza kuwa kwa sasa serikali inafanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003 ili iweze kuendana na mahitaji ya sasa ambapo mapitio ya sera hii yanaendelea.
“Tayari sera hii imeishafikishwa kwenye vyombo mbalimbali vya maamuzi na sasa tuko kwenye hatua za mwisho za kukusanya maoni ya mahitaji ya wazee ili yaweze kujumuishwa kwenye sera hiyo,” alisema.
Alisema serikali bado inatambua kuwepo kwa changamoto ya upatakinaji wa Sheria ya wazee, pensheni kwa wazee na upatikanaji wa dawa za wazee katika baadhi ya vituo vya afya mambo ambayo Serikali inaendelea kuyafanyia kazi.
“Natambua pia kuwa sera ya wazee imekaa muda mrefu bila kutungiwa sheria. Hata hivyo naomba kuwatoa wasiwasi wazee wangu kuwa tunaendelea na jitihada za kuhakikisha upatikanaji wa sheria ya wazee,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Taifa, Lameck Sendo, alisema vitendo vya ukali kwa wazee bado vinaendelea kujitokeza nchini kutokana na kuwepo kwa imani potofu.
Alisema mfano katika kijiji cha Kisharika waliuawa wazee watatu ambao ni Agnes Msengi (84), Widina Said (80) na Winfrida Ndigina (80) ambao waliuawa Machi 26, 2022 kutokana na imani za kishirikina.
Sendo alisema baadhi ya waganga wa kienyeji na tiba asilia wamekuwa ni chanzo cha kutokea mauaji ya wazee kutokana na kuleta hofu kwa jamii kutokana lamli chonganishi wanazofanya.
“Nitowe ushauri kwa SMAUJATA (Kampeni ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii) ambayo inasaidia kupinga ukatili dhidi ya wanawake, wazee na watoto pamoja na kazi ya wanayoitoa elimu hiyo pia iwafikie na waganga wa kienyeji” alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri wa Wazee Manispaa ya Singida, Juma Mudida, alihoji kwanini watuhumiwa wa mauaji ya wazee wa Kijiji cha Kisharita hawajapatikana hadi leo.
“Dhahabu iko chini ardhi mamilioni ya kilomita na inapatikana, inakuweje inashindikana hadi sasa kupatikana kwa watuhumiwa waliosababisha vifo vya wazee hao,” alisema.
Naye Programu Meneja wa Shirika la HelpAge Tanzania, Joseph Mbasha, alisema shirika lake limekuwa likishirikiana na halmashauri 23 katika kupinga vitendo vya ukatili na manyanyaso dhidi ya wazee, kuboresha upatikanaji wa huduma za afya zilizo rafiki na bora kwa wazee.
Mbasha alisema afu nyingine zinazotekelezwa kwa kushirikiana na halmashauri ni kutoa huduma jumuishi wakati wa majanga, kuhakikisha usalama wa kipato na kuchagiza harakati za mabadiliko.