Na Mwandishi wetu, Babati
MWENGE wa uhuru umepita katika miradi mitano na kuzindua miradi miradi miwili, kuweka jiwe la msingi miradi miwili na kuona na kukagua mradi mmoja yote ya thamani ya shilingi bilioni 1.1.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Anna Mbogo, ameyasema hayo wakati akimkabidhi mwenge wa uhuru Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Babati Anna Fissoo kwenye eneo la Singu.
Mbogo amesema mwenge wa uhuru umekimbizwa umbali wa kilomita 150.8 kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Babati na kupita Tarafa mbili, Kata tano na vijiji 10 na kupitia miradi mitano ya thamani ya Tshs 1,077,262,620.66.
Amesema miradi hiyo imegusa mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu, afya, maji, viwanda na uwezeshaji wa makundi maalum.
“Pamoja na kupitia miradi ya maendeleo, mwenge wa uhuru umekimbizwa ukiwa unaelimisha na kueneza ujumbe mahsusi na kugusia masuala mtambuka ya uzingatiaji wa lishe bora, kupambana na VVU/UKIMWI, Rushwa, Malaria na dawa za kulevya.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa Sahili Nyanzabara Geraruma amewapongeza Mkuu wa Wilaya ya Babati Lazaro Twange, Mkurugenzi Mbogo, madiwani wataalam na wananchi kwa kuutendea haki mwenge wa uhuru ukiwa kwenye eneo lao.
“Pamoja na mwenge kuridhia kupitisha miradi yenu mnapaswa kutekeleza maagizo yote tuliyotoa ikiwemo kufanyia kazi ujumbe wa mwenge wa uhuru wa mwaka huu,” amesema Geraruma.
Ujumbe mahsusi wa mwenge wa uhuru mwaka 2022 ni ‘Sensa ni msingi wa mipango ya maendeleo, shiriki kuhesabiwa, tuyafikie maendeleo ya Taifa’