***********************
Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Simon N. Sirro, tarehe 15.06.2022 alifanya uhamisho wa baadhi ya maofisa kwa lengo la kuboresha ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Polisi.
Waliohamishwa ni Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) William F. Mkonda aliyekuwa Kamanda wa Polisi Tarime Rorya anayekwenda kuwa Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalum ya Dar es Salam (ZTO) akichukua nafasi ya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Abdi H. Isango ambaye anakwenda kuwa Mkuu wa Operesheni Mkoa wa Mbeya.
Pia amemuhamisha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Zuberi Mwombeji ambaye alikuwa Mkuu wa Operesheni Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwenda Makao Makuu ya Polisi kuwa Mkuu wa Kitengo cha Ustawi wa Jamii na Uchumi, na nafasi yake inachukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Kennedy P. Mgani ambaye alikuwa Mkuu wa Operesheni Mkoa wa Mbeya.
Aidha amemuhamisha Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Pipi J. Kayumba kwenda Mkoa wa Singida kuwa Afisa Mnadhimu namba moja na nafasi yake inachukuliwa na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Tarcis M. Idelfonce ambaye alikuwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Dodoma.
IGP Sirro pia amemhamisha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Jumanne I. Juke aliyekuwa Mkuu wa Polisi wilaya ya Geita kwenda kuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi Rufiji kuchukua nafasi ya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ame A. Anoqie ambaye amehamishiwa Tarime Rorya kuwa Afisa Mnadhimu namba Moja kuchukua nafasi ya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Geofrey B Sarakikya ambaye anakuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya.