Na Dotto Mwaibale, Ikungi
BARAZA la Watoto Wilaya ya Ikungi mkoani Singida limesema wazazi kutokuwa
karibu nao kunasababisha mmomonyoko wa maadili huku wakikumbwa na vitendo vya ukatili dhidi yao.
Hayo yameelezwa jana na watoto kutoka shule mbalimbali za wilaya hiyo
wakati wa kuanzisha na kuhuisha mabaraza hayo ambayo yapo kwa mujibu wa sheria
za nchi na kimataifa.
Akizungumza katika baraza hilo kwa niaba ya wenzake mtoto Kauthal Ismail
kutoka Shule ya Sekondari ya Irisya alisema
baada ya kujifunza kuhusu ulinzi wa mtoto amegundua kwamba wazazi wengi
hawawalindi watoto wao hususani wanaosoma katika shule za mbali.
“Unakuta wazazi wengi watoto wao wanaosoma shule za mbali wanawaacha
wanaenda wenyewe shuleni na wanaporudi kutoka shuleni wanachelewa kurudi
nyumbani lakini wazazi hawawaulizi ni kwa nini wamechelewa” alisema
kauthel.
Kauthel alisema kitendo cha mzazi kutokumuuliza mntoto wake sababu za
kuchelewa kurudi nyumbani wakati wa kutoka shule kinawapa mwanya kujiingiza
kwenye vitendo viovu visivyo na maadili.
Awali akifungua mabaraza hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya
ya Ikungi, Justice Kijazi alisema mabaraza ya watoto ni chombo kilichoundwa
kisheria kwa sera ya watoto ya mwaka 2008.
Alisema baraza ya watoto ni chombo cha uwezeshaji cha kujifunza masuala
yanayohusu haki za mtoto hivyo wanapaswa kukitumia ili kiweze kuwasaidia katika
kulinda haki zao.
Kwa upande wake Afisa wa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ikungi, Haika Massawe
alisema mabaraza hayo ni chombo muhimu ambacho kinawawezesha watoto kutoa
changamoto zao mbalimbali ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.
“Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi imekuwa na dhamira ya kuwakutanisha watoto katika chombo kimoja kujadili changamoto zinazowakabili na kushiriki namna ya kuzitatua jambo ambalo litafanikiwa kwa uwepo kwa baraza lili la watoto wilayani kwetu” alisema Massawe.
Katika ufunguzi wa baraza hilo mada zinazowahusu watoto zilitolewa na wawezeshaji mbalimbali.