Vodacom Tanzania Plc imeanza kutoa mgao wa Shilingi 3.3 bilioni kwa watumiaji wake zaidi ya 7.7 milioni, ikiwa ni sehemu ya faida iliyopatikana kwenye akaunti za M-Pesa. Malipo haya yanategemewa kukamilika tarehe 17 Juni, ambapo wateja wote watakuwa wameshapokea mgao wao na kufanya idadi itakayotolewa kwa ujumla kufikia Shilingi 174 bilioni tangu kampuni hiyo ianze kugawa faida kwa wateja wake
Akifafanua kuhusu gawio hilo la M-Pesa, Mkurugenzi wa M-Pesa Epimack Mbeteni, alisema, “tuna furaha kubwa sana kuona kuwa huduma ya M-Pesa inaendelea kuwa msingi wa shughuli za kibiashara pamoja na maisha ya kila siku ya wananchi hapa nchini. Tuko katika mchakato wa kugawa Shilingi 3.3 bilioni kwa wateja wetu ambao wamekuwa wakitumia mfumo wetu kwa kipindi hiki, na malipo yanaingia moja kwa moja katika akaunti zao za M-Pesa.”
Faida italipwa kwa wateja, mawakala, wakala mkuu na wadau wengine wa kibiashara wa M-Pesa kulingana na matumizi yao ya huduma za M-Pesa. Gawio linategemea kiasi cha matumizi ya huduma katika kipindi hicho cha robo ya kwanza ya mwaka 2022 (Januari hadi Machi). Shughuli hizo ni pamoja na kuhamisha pesa, kulipa bili, manunuzi ya muda wa maongezi na mengine.
Wateja wanaweza kutuma neno “KIASI” kwenda namba 15300 ili kuona kiasi cha gawio watakalopokea. Mara baada ya kupokea mgao, wateja wa M-Pesa wanaweza kutumia gawio hilo kwa njia ya kutoa pesa taslimu, kununua vifurushi vya maongezi na data au kutumia kulipia bili au manunuzi ya bidhaa.
Bw. Mbeteni alimalizia kwa kusema, “Mfumo huu wa kipekee umekuwa na nafasi kubwa katika kujenga hali ya ushirikishwaji na upatikanaji wa huduma za kifedha nchini. Wanawake na vijana wameona unafuu na urahisi wa kutumia M-Pesa na wanatumia huduma nyingi ili kuboresha maisha yao. Pia mfumo umekuwa rasilmali muhimu katika kuwezesha biashara ndogondogo na kupambana na changamoto zilizosababishwa na mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO -19. Kwetu Vodacom Tanzania, dhamira yetu ni kuhakikisha kuwa mfumo huu tunauboresha ili kuendana na mahitaji ya wateja wetu.”
Kuhusu Mfumo wa Vodacom M-Pesa
Vodacom M-Pesa ni mfumo mkubwa kabisa nchini wa huduma za kifedha kwenye mtandao wa simu uliozinduliwa na Vodacom Tanzania Plc mwaka 2008. Kwa sasa ukiwa umesajiliwa na shirika la GSMA na ukiwa na watumiaji zaidi ya 11 milioni, M-Pesa imeongeza kwa kiasi kikubwa ushirikishwaji kifedha pamoja na shughuli za kiuchumi nchini. Wateja wanaweka na kutoa pesa kutoka kwenye akaunti zao za M-Pesa kupitia mtandao wa mawakala Zaidi ya 108,000 nchi nzima. Mtandao wa M-Pesa unaunganisha biashara, mabenki na taasisi za serikali katika kuwezesha miamala kidijitali.