**************************
Wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Arusha, wametakiwa kuwa Mabalozi wazuri kwa vijana wenzao kwa kuhakikisha kuwa elimu ya Miliki Ubunifu inawafikia vijana wengi.
Afisa Mwandamizi kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Raphael Mtalima ametoa wito huo mapema leo tarehe 15 Juni, 2022 Jijini Arusha, wakati akitoa elimu ya Miliki Ubunifu chuoni hapo yenye lengo la kuwajengea uwezo.
Bw. Mtalima ameeleza kuwa wanafunzi hao wanapaswa kuwa mawakala wazuri kwa kufikisha elimu ya Miliki Ubunifu katika jamii inayowazunguka na mahali popote watakapokwenda .
Amesisitiza kuwa wakiielewa elimu hiyo inayotolewa na BRELA, itakuwa rahisi kuisambaza kwa jamii kwa ujumla.
Bw. Mtalima amesema BRELA kwa sasa imejikita kutoa elimu ya Miliki Ubunifu katika Vyuo Vikuu na vya Kati lengo likiwa ni kuzalisha kizazi chenye uelewa mzuri wa Ubunifu.
“Vyuo vingi vya ufundi kazi zao nyingi ni za Ubunifu hivyo elimu hii itawahamasisha na kutambua umuhimu wa kurasimisha bunifu zenu mnazozivumbua,” amefafanua Bw. Mtalima.
Aidha Bw. Mtalima amesema kuwa utoaji wa elimu hiyo vyuoni utawapatia vijana fursa ya kuzidi kuvumbua kwani kwa sasa vijana wengi wamekuwa na weledi wa kutosha na chachu kubwa ya kujifunza.
Ameongeza kuwa baada ya kupata elimu hiyo wanatakiwa kuwasilisha BRELA vumbuzi zao kupitia mfumo wa Usajili kwa njia ya mtandao(ORS) unaopatikana katika tovuti ya BRELA, www.brela.go.tz