Kaimu Afisa mtendaji mkuu wa Atamizi ya DTBi,Dokta Erasto Mlyuka akizungumza katika mafunzo hayo jijini Arusha .
Mhadhiri msaidizi wa chuo Cha ufundi Arusha (ATC) ambaye pia ni Mratibu wa mradi huo,Busumabu Jacob akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha.
****************************
Julieth Laizer ,Arusha.
Arusha.VIJANA wanaosoma masomo ya sayansi nchini wametakiwa kutumia bunifu zao kuzalisha rasilimali mbalimbali zitakazotatua changamoto zilizopo kwenye jamii na kujiongeza kipato.
Akizungumza jijini Arusha,katika ufunguzi wa mafunzo ya siku nne ya kuendeleza bunifu kwa baadhi wanafunzi wa kidato cha sita na tano wanaosoma masomo ya sayansi katika shule saba zilizopo jijini Arusha,Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Atamizi ya DTBi,Dk.Erasto Mlyuka amesema ifike mahali vijana watumie taaluma zao wanazopata shuleni kutatua changamoto katika jamii.
“Ni vyema mkatumia mawazo yenu ya kibiashara katika kuleta suluhu ya matatizo katika jamii na kwa kufanya hivyo itawasaidieni nyinyi kutumia mwanya huo kama fursa katika kujikwamua kiuchumi kwa kujiongezea kipato,”amesema Dk.Mlyuka.
Amesema kuwa, ili nchi zipige hatua katika nyanja za sayansi na Teknolojia ni vema vijana hao wakasaidiwa katika bunifu zao ili zilete ufumbuzi wa changamoto zilizopo kwenye jamii.
Naye Meneja Mradi kutoka Kituo Atamizi cha Tume ya Sayansi na Teknolojia (DTBi) ,Josephine Sepeku amesema wameamua kushirikiana na Chuo cha Ufundi Arusha(ATC) kwa lengo la kuendeleza bunifu za wanafunzi hao kwa ili wafungue biashara zao na kuweza kuajiri wengine.
“Bunifu hizo zitakuwa ndani ya masomo ya sayansi wanayosoma shuleni ili kufikia lengo la kutatua changamoto katika jamii kupitia elimu wanayopata madarasani na kuweza kutengeneza ajira kwa wengine nakufikia Tanzania ya Viwanda,”amesema.
Naye Mratibu wa mradi huo ,Busumabu Jacob ametaja shule zilizoshiriki mwaka huu ni saba ambazo ni St.Jude,St.Mary’s Duluti,Shule ya Sekondari ya Wasichana Arusha,Ilboru,Edmund Rise na Bishop Durning na Sekondari ya Arusha.
Amesema kuwa, matarajio yao ni kuhakikisha wanafunzi hao waliopata fursa hiyo wafikie ndoto zao katika kutatua changamota katika jamii na kuzalisha ajira.
“Kwanza watapewa mafunzo kwa muda wa siku nne ili wafahamu namna ya kutumia taaluma yao kuzalisha mawazo ya kibiashara ambayo yataleta tija katika uzalishaji wa bidhaa ikiwa hadi sasa wanafunzi walioshiriki katika mradi huu ni 85, tangu uanze mwaka 2019,”amesema.
Baadhi ya wanafunzi waliopata fursa ya mafunzo hayo ya kuendelezwa bunifu zao kupitia mawazo yao ya kibiashara wamesema wamekuwa wakibuni bidhaa mbalimbali zikiwemo pembejeo za kilimo lakini haziendelezwi ila kupitia mradi huo utawasaidia kujikwamua kiuchumi pamoja na kusaidia jamii kutatua changamoto.