Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwasili katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma wakati wa Hafla ya kupokea Gawio la Serikali la shilingi bilioni 30.7 kutoka Benki ya NMB leo tarehe 15 Juni 2022.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akipokea mfano wa hundi ya shilingi shilingi bilioni 30.7 ambayo ni Gawio la Serikali kutoka Benki ya NMB katika hafla iliofanyika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma leo tarehe 15 Juni 2022.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizungumza na viongozi wa Serikali,viongozi wa Benki ya NMB pamoja na watumishi wa Benki hiyo wakati wa Hafla ya kupokea Gawio la Serikali la shilingi bilioni 30.7 kutoka Benki ya NMB iliofanyika katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma leo tarehe 15 Juni 2022.
************************
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ameagiza Mashirika ambayo Serikali ina hisa kuhakikisha yanaanza kutoa Gawio kwa serikali mara moja, pia Taasisi zinazotakiwa kutoa asilimia 15 ya mapato ghafi kwa mujibu wa sheria zifanye hivyo kikamilifu na kwa wakati.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa hafla ya kupokea Gawio la shilingi bilioni 30.7 kutoka kwa Benki ya NMB iliofanyika katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma leo tarehe 15 Juni 2022. Amesema Mashirika ambayo yanategemea ruzuku kutoka mfuko mkuu wa Serikali yanapaswa kuwa na mikakati madhubuti na inayotekelezeka ya kupunguza utegemezi kwa Serikali na kumuagiza msajili wa Hazina kuhakikisha wakuu wa taasisi husika wanatekeleza maagizo hayo.
Aidha Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuimarisha na kuweka mazingira rafiki na endelevu ya kufanya biashara katika sekta ya fedha na sekta zote nchini. Pia ameipongeza Benki ya NMB kwa kuendelea kuchangia maendeleo ya jamii nchini (corporate social responsibility) sambamba na kusaidia ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato. Amewaasa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuongeza fursa za ajira kwa vijana na wanawake pamoja na kuboresha huduma za kijamii kwenye sekta mbalimbali kama afya,elimu na utunzaji wa mazingira ikiwa ni pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na tabiawatu.
Kwa Upande wake Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Wizara itaendelea kusimamia maelekezo ya kuhakikisha taasisi za serikali na zile ambazo serikali ina hisa zinatoa Gawio. Aidha amesema serikali itaendelea kushirikiana na taasisi zote za sekta binafsi ili kuweza kuhakikisha zinafanya kazi vizuri.
Awali Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna amesema Gawio la Serikali kutoka Benki ya NMB limeendelea kukua kila mwaka na kuwa endelevu mpaka kufikia bilioni 30.7 kwa mwaka 2022 kutoka bilioni 10.48 mwaka 2018. Amesema adhma ya NMB ni kuleta tija kwa wawekezaji ikiwemo serikali ambayo inamiliki hisa za asilimia 31.8.
Aidha Bi Zaipuna ameongeza kwamba Benki ya NMB itaendelea kuwa mdau mkubwa wa serikali katika kufanikisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi hasa kupitia uwekezaji katika sekta ya kilimo na biashara. Amesema mpaka mwezi Desemba 2021 jumla ya mikopo ya shilingi Trilioni 4.3 imetolewa kwa wakulima na wafanyabiashara.