Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Ali Hamad Makame akizungumzia navyombo vya Habari.
…………………………………..
Na. Zillipa Joseph, Katavi
Wakazi wa mkoa wa Katavi wamekemea vikali tabia mbovu inayoendelea kufanywa na baadhi ya watu ya kuwadhalilisha watoto kingono.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti wakazi hao wamelitaka Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wote watakaokamatwa kwa makosa hayo.
‘Kwakweli mimi kama mzazi huwa naumia sana kila ninaposikia mtoto amebakwa au wamemwendea kinyume na maumbile’ alisema Grace Mutayoba mkazi wa Makanyagio katika Manispaa ya Mpanda.
‘Zamani tulikuwa tukivisikia vitendo hivyo katika miji mikubwa kama Dar es Salaam lakini sasa hata huku kwetu kila kukicha unasikia’ aliongeza.
Bwana Baraka Gervas mfanyabiashara katika soko la Buzogwe ameishauri serikali kuongeza adhabu kwa watu watakaopatikana na hatia kwa makosa hayo. Amesema matukio hayo mara nyingi ukiyasikia yanaambatishwa na imani za kishirikina jambo ambalo halipendezi na linaharibu maisha ya waathirika.
Chifu wa Kabila la Wakonongo bwana Charles Mallac ameitaka jamii pia kuwa na ushirikiano mkubwa na vyombo vya sheria pale tukio kama hili linapotokea.
Chifu Mallac amesema hayo kufuatia kesi nyingi za ubakaji na ulawiti kushindwa kufika mwisho kwa sababu ya wazazi kushindwa kutoa ushahidi na wakati mwingine wamekuwa wakipokea malipo kutoka kwa wabakaji ili kuyamaliza kimya kimya.
Hivi karibuni Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi Kamishna Msaidizi wa Polisi Ali Hamad Makame alitoa taarifa ya tukio la mtoto wa umri wa miaka mitano kubakwa na kulawitiwa.
Katika tukio hilo lililotokea tarehe 13 Juni majira ya saa kumi na mbili jioni katika kijiji cha Kagunga kilichopo kata ya Kasekesese wilayani Tanganyika mkoani Katavi mkazi mmoja wa kijiji hicho Juma Jackson mwenye umri wa miaka 30; alimbaka na kumlawiti mtoto wa kike mwenye umri wa miaka mitano.
Kamanda Makame ameeleza kuwa mtuhumiwa alimvizia mtoto huyo ambaye alikuwa akitoka nyumbani kwao kuelekea kwa jirani ambapo alimvutia vichakani na kumfanyia vitendo hivyo haramu huku akimkaba shingo na kumtisha asipige kelele la sivyo atamuua.
‘Baada ya uchunguzi wa awali imebainika kuwa mtuhumiwa alifanya kitendo hicho kwa imani za kishirikina kwani aliahidiwa kulipwa ng’ombe watatu akikamilisha kazi yake’ alisema Kamanda
Kamanda Makame ameeleza kuwa mtuhumiwa aliambiwa akimaliza kufanya kitendo hicho akamuogeshe mtoto huyo katika shamba la mtu aliyemtuma kama zindiko la shamba.
Kufuatia kitendo hicho Kamanda huyo wa Polisi mkoa ameendelea kutoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano ili kuvitokomeza vitendo vya ukatili wa kingono dhidi ya watoto.
Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia mkoa wa Katavi Jackson Fuime amesema matukio hayo yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara ambapo kwa mwezi mmoja wastani wa watoto sita hadi saba hufanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono.
Fuime ameeleza kuwa matukio hayo mara nyingi yanafanywa na watu walio karibu na familia na hivyo kuitaka jamii kuongeza umakini katika ulinzi wa watoto wao.
‘Wakati mwingine unapokea kesi ya mjomba kumlawiti mpwa wake ukiangalia mazingira ya tukio unakuta wanalala chumba kimoja mtu mzima na mtoto’ alisema
Bi. Anna Shumbi ni Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Katavi, amesema ifike mahala jamii zetu ziache kuoneana aibu kwani matukio mengi hayaripotiwi kwa sababu za kuhofia kuchekwa.
‘Unakuta mama anaona nikisema ni shemeji yangu kambaka mtoto majirani watanicheka’ alisema