Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wakiwa katika kikao maalum cha Baraza hilo cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kilichofanyika kwenye ukumbi wa shule ya sekondari Kigonsera na kuongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge
…………………………………………….
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma imechangia Zaidi ya shilingi milioni 240 kwenye mfuko wa wanawake wa uwezeshaji vijana na wenye ulemavu.
Akizungumza kwenye kikao maalum cha Baraza la madiwani cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG kwa mwaka 2020/2021 kwenye ukumbi wa Sekondari ya Kigonsera,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge imeipongeza Halmashauri kwa kuchangia kwa asilimia 92 kwenye mfuko huo wenye vikundi 13.
Kati ya fedha hizo kundi la wanawake limepata Zaidi ya shilingi milioni 108,vijana Zaidi ya shilingi milioni 106 na kundi la wenye ulemavu ni shilingi milioni 25.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,pia ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa kuweza kukusanya mapato ya ndani kwa asilimia 77 ya lengo la kukusanya Zaidi ya shilingi bilioni nne ambapo Halmashauri hiyo imeweza kukusanya Zaidi ya shilingi bilioni tatu.
“Kwa mwaka wa fedha 2019/2020 hamkufia kile kiwango cha angalau asilimia 81 hivyo nawapa hongera kwa kiasi,lakini nawatia shime ongezeni jitihada za kukusanya na kuhakikisha Halmashauri yenu inafikia lengo la kitaifa la kukusanya kuanzia asilimia 81’’,alisisitiza RC Ibuge.