Naibu waziri wa afya ,Dokta Godwin Mollel akizungumza wakati akiwa katika ziara hiyo jijini Arusha.
*******************************
Julieth Laizer,Arusha.
Arusha.NAIBU Waziri wa Afya Dk.Godwin Mollel ameziomba Taasisi za dini nchini,kujenga vituo vingi vya afya ili kuisaidia serikali utoaji wa huduma za afya na ajira.
Aidha,amewataka watumishi wa afya nchini, kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wagonjwa, kwa kuzingatia weledi na kufuata maadili ya uuguzi.
Akizungumza jijini Arusha Dk.Mollel wakati wa ziara yake ya kutembelea vituo vya afya, ikiwemo Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) na Hospitali ya Mkoa Mount Meru amewapongeza watumishi kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuwataka kuendelea kutoa ushirikiano pindi serikali inapowahitaji katika kutimiza malengo waliyojiwekea.
“Nawaomba Taasisi za dini mtusaidie kujenga zaidi vituo vya afya ili wananchi wapate huduma za afya bila kuhangaika au kufuata mbali,lakini hii itasaidia pia kutoa ajira kwa wananchi,”amewapongeza.
Amesema kuwa, watumishi wa afya wametakiwa kuwa kioo cha jamii kwa kutoa huduma zenye upendo kwa wagonjwa na kuacha lugha za matusi.
Dk.Mollel amesema kuwa, katika kipindi cha Uviko-19 Hospitali ya ALMC maarufu kwa jina la Selian, ilitoa msaada mkubwa wakati Hospital ya Mkoa ya Mount Meru ilipozidiwa na wagonjwa, katika utoaji wa huduma kwa watalii pindi walipopata changamoto ya afya .
Amesema kuwa,hiyo ni faida kwa Taasisi za dini zinapojenga hospitali kwani wanaisaidia serikali utoaji wa huduma hizo kama ilivyotokea katika kipindi cha janga hilo.
“Hakika hapa kila mmoja aliona umuhimu wa Taasisi hizi za dini kujenga hospitali au vituo vya afya, kwani isingekuwepo ALMC katika janga la Uviko-19 hali ingekuwa mbaya kwa wagonjwa waliokumbwa na janga hilo,maana wagonjwa wangefurika hospitali ya serikali,”amesema .
Pia,Dk.Mollel amewapongeza watumishi wa ALMC kwa hatua waliyofikia kutoka bajeti ya dawa ya Sh.milion 70 hadi kufikia bajeti ya Sh.milioni 119.
“Nimefurahishwa na utendaji kazi wenu sasa nataka ifikapo mwaka 2023 bajeti yenu ya dawa Ifike Sh.milioni 250 na ili mtimize malengo yenu endeleeni kufanya kazi kwa umoja,”amesema.
Aidha ameutaka uongozi wa ALMC kuboresha hospital hiyo na utoaji huduma zao, huku akihimiza umuhimu wa kuepuka migogoro.
Mkurugenzi wa Hospitali ya ALMC, Elisha Twisa amesema kuwa changamoto ya uviko 19 imeathiri hospitali hiyo kwa sehemu kubwa kwa kuwa wagonjwa wengine walishindwa kulipa gharama za matibabu,kutokana na mitungi ya oksijeni kuwa na gahrama za juu.
Amesema licha ya hospitali hiyo kutoa huduma bora bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo madeni yaliyosababisha kuchelewa kulipwa kwa mishahara ya watumishi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya ALMC, John Hillary amesema hospitali hiyo ina malengo makubwa likiwemo la kujenga hospitali kubwa itakayohudumia watalii.