****************************
Na Mwandishi wetu, Manyara
MWENGE wa uhuru umeingia Mkoani Manyara na utatembelea miradi 39 ya maendeleo yenye thamani ya sh23.2 bilioni na unatarajiwa kukimbizwa mzunguko wa kilometa 1,208.2.
Mkuu wa mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere akipokea Mwenge wa uhuru mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro kutoka kwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Stephen Kagaigai, amesema utakimbizwa kwenye halmashauri saba.
Makongoro amesema mwenge wa uhuru utakimbizwa kwenye halmashauri za Simanjiro, Kiteto, Babati mji, Babati wilaya, Hanang’ Mbulu wilaya na Mbulu mji.
Amesema ukiwa mkoani Manyara, mwenge wa uhuru utaweka mawe ya msingi miradi 17 ya thamani ya sh20.7 bilioni, kuzindua miradi 13 ya thamani ya sh1.6 bilioni na kukagua na kuona miradi tisa yenye thamani ya sh843.7 milioni.
“Mchanganuo wa gharama hizo za miradi ni nguvu ya wanachi sh399.9 milioni, serikali kuu sh21.6 bilioni, halmashauri sh403.5 milioni na wadau wengine wamechangia sh764.6 milioni,” ameema Makongoro.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Dk Suleiman Serera amesema ukiwa eneo hilo mwenge wa uhuru utatembelea miradi sita ya thamani ya sh1.3 bilioni.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru mwaka 2022, Sahili Nyanzabara Geraruma amesema ujumbe mahsusi ni sensa ni msingi wa mipango ya maendeleo, shiriki kuhesabiwa, tuyafikie maendeleo ya Taifa.