Mkurugenzi wa uendeshaji wa Kampuni ya Nalika Safaris Ltd Frank Laizer, akionesha baadhi ya magari yatakayotumika kwa ajili ya shughuli za utalii katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Tunduru na mikoa ya kusini.
Baadhi ya magari ya kampuni ya Nalika Safaris Ltd yakiwa tayari kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kitalii kwenye vivutio vilivyopo katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma na mikoa mingine ya Kusini.
Picha zote na Muhidin Amri
…………………………………………………………………………………
Na Muhidin Amri,Tunduru
JITIHADA za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan za kutangaza vivutio vya utalii kupitia Filamu ya Royal Tour, zimeanza kuzaa matunda baada ya Kampuni ya Nalika Safaris ltd kuamua kuanzisha shughuli zake za utalii katika mji wa Tunduru ukiwa ndio makao makuu ya kampuni hiyo.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Kampuni hiyo Frank Laizer alisema, wamekuja wilayani Tunduru kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza utalii wa nchi yetu ndani na nje ya nchi anazozifanya kupitia Programu ya The Tanzania- Royal Tour.
Alisema,kwa muda mrefu sekta ya utalii imekuwa ikitangazwa sana katika mikoa ya Kaskazini, lakini Nalika Safaris imeona upo umuhimu wa kuwekeza na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika mikoa ya kusini hususani wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.
Alisema,wamejipanga kuhakikisha kampuni yao iwe moja ya vyanzo vikubwa vya mapato kwa wilaya ya Tunduru na kuwa mlipa kodi na sio kama makampuni mengine ambayo huacha mapato na kodi zake katika mikoa mingine na kuja kuacha sehemu ndogo tu ya mapato yao katika wilaya ya Tunduru.
Kwa Mujibu wake, kuanzishwa kwa kampuni hiyo wilayani humo,kutasaidia sana kutangaza vivutio vilivyopo Tunduru,na kuchangia mapato ya Halmashauri ya wilaya ya Tunduru na hivyo kuwa sehemu ya wadau wakubwa wa maendeleo na kutoa ajira za muda na za kudumu kwa baadhi ya Wananchi ambao watapata fedha kwa ajili ya kuendesha maisha yao ya kila siku.
Laizer, amewaomba wakazi wa Tunduru, serikali na wadau wengine kuwapa ushirikiano katika jitihada zao za kutangaza utalii na kufungua fursa mbalimbali kwani Kampuni hiyo ni ya wazawa(Watanzania)kwa asilimia mia moja na ya kwanza kufungua ofisini zake wilayani humo.
Aidha alisema, hatua ya kampuni ya Nalika Safaris kufungua ofisi katika wilaya hiyo ni kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan za kutangaza vivutio vya utalii na kuwataka Watanzania kutumia fursa hiyo kuwekeza katika sekta ya utalii katika mikoa ya kusini ambayo kwa muda mrefu imesahaulika.
Laizer amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi anazozifanya kuitangaza Tanzania Kimataifa kupitia Programu ya Tanzania-The Royal Tour na kuhaidi kwamba, kampuni ya Nalika Safaris itakuwa bega kwa bega na jitihada hizo kutangaza utalii na kuvutia uwekezaji wa maslahi ya nchi yetu.
Alisema, mpango wao ni kufanya utalii wa aina zote zinazopatikana katika mikoa ya kusini ikiwamo utalii wa picha, kutembelea maeneo ya Kihistoria, utalii wa uvuvi kwenye mto Ruvuma
ziwa Nyasa na maeneo maaarufu ya mto Mwambesi pamoja na uwindaji wa kitalii.
Laizer ameiomba Serikali, kufikiria kujenga uwanja wa ndege wilayani humo ili kurahisisha huduma ya usafiri kwa wageni wa ndani na nje ya nchi ambao mara nyingi wamekua wakitamani kufika wilayani humo lakini wanashindwa kutokana na umbali wa kutoka kwenye viwanja vikuu vya ndege.
Ameeleza kuwa kwa kutumia usafiri wa ndege ni masaa mawili tu kutoka Dar es salaam hadi Tunduru ambapo tayari ni karibu sana na vivutio vingi vilivyopo katika mikoa ya kusini tofauti na sasa ambapo kwa kutumia njia ya barabara ni safari ya siku nzima jambo ambalo kila mtalii anajaribu kulikwepa.
Amewataka wakazi wa Tunduru kujianda kupata mambo mazuri kutokana na uwekezaji wa utalii utakaofanywa na kampuni hiyo ya Nalika Safaris Ltd.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Uhifadhi Wanyamapori ya Nalika Safaris Said Masoud amepongeza jitihada kubwa inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kutangaza vivutio vya utalii na kuvutia watu mbalimbali kwa ajili ya
Kuwekeza katika sekta ya utalii hapa nchini.
Akizungumzia kuanzishwa kwa kampuni ya Wazalendo ya Nalika Safaris alisema, huo ni mwanzo mzuri ndani ya wilaya ya Tunduru na mkoa wa Ruvuma ambao umebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi ambazo bado hazijatangazwa vya kutosha.
Alisema, kufunguliwa na kuanzishwa kwa kampuni ya Nalika Safaris wilayani humo kunaonyesha mwanga mkubwa kwa maendeleo katika wilaya ya Tunduru na mikoa ya kusini kwa ujumla ambayo kwa muda mrefu iko nyuma katika masuala ya utalii ukilinganisha na mikoa ya Kaskazini na Pwani.
Ameomba makampuni mengi zaidi kwenda kufungua ofisi zao wilayani Tunduru, ili kuongeza nguvu kutangaza utalii katika mikoa ya kusini.
Masoud, ameiomba Serikali kupitia wizara ya maliasili na utalii ihakikishe inatoa elimu ya kutosha kwa wananchi wanaoishi katika vijiji vinavyozungukwa na hifadhi za Wanyamapori juu ya umuhimu wa rasilimali zilizopo ili kuepuka migogoro iliyopo kati ya hifadhi na wananchi.
Mkazi wa kijiji cha Rahaleo Asha Ching’amba alisema, hiyo ni fursa kubwa kwa wananchi wa wilaya hiyo ya Tunduru kuanza kunufaika na rasilimali za misitu na wanyamapori na kuhaidi kutumia nafasi hiyo kujikwamua na umaskini.