Mkuu wa wilaya ya Igunga mkoani Tabora Sauda Mtondoo (kushoto) akimkabidhi funguo ya pikipiki afisa ugani kata ya Nanga Ambele Mwangomo (kulia)
………………………
Na Lucas Raphael ,Tabora
Mkuu wa wilaya ya Igunga mkoani Tabora Sauda Mtondoo amewaonya maafisa ugani wataokaogeuza pikipiki za serikali walizopewa kwa ajili ya kuwahudumia wakulima kuwa bodaboda.
Mkuu huyo wa wilaya alitoa onyo hilo wakati akikabidhi pikipiki 23 kwa maafisa ugani wa halmashauri ya wilaya ya Igunga zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kuwawezesha maafisa ugani kuwafikia wakulima katika maeneo yao ya kazi.
Alisema kila afisa ugani ana wajibu wa kuhakikisha pikipiki aliyopewa anaitumia kwa shughuli iliyokusudiwa ikiwa ni pamoja kuwahudumia wakulima kwani itasaidia wakulima kutokuwa na manung’uniko ya kutofikiwa na maafisa hao wa ugani.
“ ndugu zangu maafisa ugani naomba mnielewe msimuangushe Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassani kwani amefanya kazi kubwa ya kusaidia sekta ya kilimo kuwa na usafiri hivyo basi nategemea kupitia vyombo hivi vya usafiri mlivyopata mtaenda kufanya kazi kubwa ya mapinduzi ya kilimo”.
Hata hivyo alisisitiza kuwa afisa ugani yoyote atakayebainika kugeuza matumizi kwa kutumia pikipiki hiyo kuwa bodaboda atanyang’anywa ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa hatua ya kinidhamu.
Aidha mkuu huyo wa wilaya aliwaasa maafisa ugani kuzungatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.
Nae afisa kilimo umwagiliaji na ushirika wilaya ya Igunga Grace Mkinda akitoa taarifa kwa mkuu wa wilaya ya ya Igunga kwa niaba ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Igunga Fatuma Omary alisema halmashauri ya wilaya ya Igunga ina tarafa nne ikiwemo Igunga, Igurubi, Manonga, na Simbo huku akiongeza kuwa ina kata zipatazo 35 ambazo kata ya 14 ndizo zinazohudumiwa na maafisa ugani kilimo.
Huku akibainisha kuwa kuna upungufu wa maafisa ugani kilimo 21 wa kata hizo, kutokana na upungufu huo wamekuwa wakiwatumia maafisa ugani mifugo kuhudumia wakulima wa kata ambazo hazina wataalamu.
Hata hivyo alisema halmashauri ya wilaya ya Igunga ina vijiji 119, vijiji viwili kati ya vijiji 119 vinahudumiwa na maafisa ugani kilimo kwa hiyo kuna upungufu wa maafisa ugani kilimo 117 katika vijiji 117.
Sambamba na hayo aliwasisitiza maafisa ugani utandaji kazi kwenye maeneo yao ili kuleta ufanisi katika sekta hiyo pia aliwaasa kuongeza nidhamu katika utendaji kazi zao siku hadi siku.
Kwa upande wao baadhi ya maafisa ugani waliopatiwa pikipiki hizo, Jamilla Issa wa kata ya Igunga, Ambele Mwangomo afisa ugani kilimo kata ya Nanga, Twalib Ngahoma kata ya Itumba na Claudia Mlowe wa makao makuu ya halmashauri Igunga.
Kwa nyakati tofauti walisema kwanza wanamshuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kuwapatia usafiri kwani muda mrefu wamekuwa wakipata shida kuwatembelea wakulima lakini kwa sasa wanakwenda kufanya mapinduzi makubwa ya kilimo yatakayosaidia kuongeza uzalishaji wa mazao kwa wakulima wa halmashauri ya wilaya ya Igunga.
Nae wakili mwandamizi wa serikali ya halmashauri ya wilaya ya Igunga Leopold Kaswezi alisema halmashauri ya wilaya ya Igunga itahakikisha inawafuatilia kila siku maafisa ugani wote waliopewa pikipiki hizo na atakayebainika kutumia usafiri huo kinyume na maelekezo ya serikali hawatasita kuchukua hatua kali za kisheria.