*********************
Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) imetenga kiasi cha shilingi bilioni 69.6 kwa ajili ya kutekeleza miradi 27 ya ujenzi na ukarabati wa vivuko kote nchini kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Hayo yamebainishwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala huo Lazaro N. Kilahala wakati akifanya mahojiano maalumu na maafisa wa habari kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuhusu namna ambavyo TEMESA itatekeleza miradi yake kupitia Bajeti ya shilingi Trilioni 3.8 ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ambayo imepitishwa hivi karibuni na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kilahala amesema miradi hiyo ni pamoja na ununuzi wa vivuko vipya saba, miradi ya ukarabati wa vivuko vinavyoendelea kutoa huduma, pamoja na miradi ya ujenzi wa miundombinu ya vivuko.
‘’Mpaka sasa miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 27.25 ya ununuzi wa vivuko vipya tayari imekwishasainiwa mikataba, miradi hiyo ni pamoja na ule wa Kisorya Rugezi pale Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza, kuna mradi wa Mafia Nyamisati pale Wilayani Mafia Mkoani Pwani, kuna Ijinga Kihangala Wilayani Magu Mkoani Mwanza pamoja na Nyakarilo Kome Mwanza’’. Alisema Mtendaji Mkuu na kuongeza kuwa kuna mradi wa ujenzi wa kivuko kipya eneo la Buyagu Mbalika Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza ambapo amesema mradi huo upo kwenye bajeti na pesa imekwishatenga kwa ajili ya kuanza hatua za manunuzi ya ujenzi wa kivuko hicho.
Aidha, Kilahala ameongeza kuwa TEMESA inaendelea na zoezi la ukarabati wa vivuko kote nchini ikiwa ni muendelezo wa utaratibu wa kawaida wa Serikali kuvifanyia vivuko vyote ukarabati kila inapopita miaka minne hadi mitano ili kuviwezesha kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi vikiwa katika hali ya usalama.
‘’Pale Magogoni kwa mfano, mwaka huu, Serikali tayari imekwishatoa shilingi Bilioni 4.4 kwa ajili ya kukifanyia ukarabati mkubwa kivuko cha MV. KAZI na kazi ya ukarabati inaendelea, lakini pia Serikali imetenga kwenye bajeti kwa mwaka unaoanza Julai baada ya kivuko cha MV. KAZI kurudi kutoa huduma, tunakwenda kukitoa kivuko cha MV. MAGOGONI kwa ajili ya kukifanyia matengenezo makubwa’’. Alimaliza Mtendaji Mkuu
Vivuko vilivyofanyiwa ukarabati mpaka sasa ni pamoja na kivuko cha MV. TEMESA, MV. Sengerema, MV. Tegemeo (Mwanza), MV. Kigamboni (Dar es Salaam) pamoja na MV. Mafanikio (Mtwara).
Aidha Vivuko ambavyo vinaendelea kufanyiwa ukarabati na vingine kusubiri kufanyiwa ukarabati ni pamoja na vivuko vya MV. Kitunda (Lindi), MV. Tanga (Pangani Tanga), MV. Ruhuhu (Ruvuma), pamoja na vivuko vinavyofanya kazi kwenye ziwa Victoria kikiwemo kivuko cha MV. Sabasaba, MV. Nyerere, MV. Misungwi (Mwanza) pamoja na MV. Musoma (Mara).
Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) unasimamia jumla ya vivuko thelathini na tatu katika vituo ishirini na mbili kote nchini na hivyo ujenzi wa vivuko hivyo ukikamilika itakuwa na idadi ya vivuko arobaini inavyovisimamia.