**********************
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi(UWT)Mkoa wa Njombe Scholastila Kevela amesema hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzitaka Mamlaka zinazohusika na ukusanyaji wa ushuru pamoja na kodi mbalimbali kuacha ukusanyaji wa Kodi ya miaka ya nyuma kwawafanyabiashara ni jambo linalopaswa kupongezwa.
Kauli ya Mwenyekiti huyo inakuja siku moja mara baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa agizo hilo kwa mamlaka hizo wakati akiwahutubia wananchi mbalimbali katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Kaitaba Mjini Bukoba.
Hatua hiyo ya Rais Samia ilitokana na maombi ya wafanyabiadhara wa Bukoba yaliyowasilishwa na Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini Stephen Byabato kuhusu kilio na manung’uniko ya wafanyabiashara wa mkoa huo kuhusu kutozwa kodi ya miaka iliyopita kitendo kilichoonekana kuwaumiza kutokana na Ukubwa wa madeni.
Alisema Mamlaka zinatakiwa kukusanya Kodi kuanzia Mwaka mmoja nyuma na kwamba kama zilikuwa hazifanyi hivyo miaka mingine ya nyuma ni uzembe wa watu waliokuwa madarakani.
“…Nataka kusema hivi, miaka yote hiyo watoza Kodi wapo, Halmashauri zipo, mmewaachia watu (Wafanyabiashara) Kodi hawakulipa, Leo hii unampelekea bili ya miaka mitano sita nyuma alipe nini? wakati ule ulikuwa wapi? kama hakulipa ndio ni kosa lakini kosa sio lake pekee hata wewe ambaye hukumfuata kuikusanya, kwahiyo kama alivyosema Mbunge achaneni na hiyo biashara, mnaloweza kufanya ni kurudi mwaka mmoja nyuma…” alisema Rais Samia.
Kutokana na kauli hiyo Mwenyekiti huyo wa UWT Scholastika Kevela alisema Rais Samia anazidi kuendeleza mazuri yake ya kulifanyia Taifa mambo makubwa kiasi cha kumfanya kila mtu kujiona kama yupo katika sayari nyingine kwa mengi mazuri anayoyafanya sasa.
“Kwa hilo sisi Wanawake wa UWT Mkoa wa Njombe tunampa zawadi kwa kumuimbia wimbo wa kibena tukisema Rais wetu ‘Aliyuyo(wa kipekee) Mnyawende, Mnyalusungu (Ana upendo na huruma) kwa wananchi wake, anafanya mambo ambayo wengi hatukuyatarajia kuwa kwa kipindi kifupi yangefanyika, anastahili kila aina ya pongezi na zaidi anaonyesha kuwa yeye ni mtu wa watu” alisema Kevela
Alisema kilio hicho kilichotolewa na wafanyabiashara wa Bukoba ndicho kilio cha wafanyabiashara wote nchini hivyo kafanya jambo kubwa ambalo kila mfanyabiashara nchini ana kila sababu ya kumpongeza.
Aidha alisisitiza kuwa kutokana na matendo yake hayo hakuna amejijengea mtaji mkubwa kwa wananchi na kwamba hakuna yeyote ambaye anaweza kumzuia kuchukua kiti cha Urais katika uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 baada ya wananchi wengi kuonyesha mapenzi naye.
“Kwa niaba ya wananchi wote wa mkoa wa Njombe hususani wanawake wa Chama Cha Mapinduzi tunamuhakikishia ushindi wa kishindo na zaidi tunasema Rais Samia mitano tena, tutahakikisha kwa nafasi aliyonayo anarejea tena mara baada ya uchaguzi wa mwaka 2025” alisisitiza Kevela