Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine akizungumzia maazimio yaliyofikiwa katika Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya OACPS uliofanyika jijini Brussels nchini Ubelgiji tarehe 8 na 9 Juni 2022 ambapo alimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika mkutano huo.
………………………………………
Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) umetenga kiasi cha Euro milioni 157 kukoppesha wadau wa kilimo katika nchi wanachama kwa masharti nafuu ili kuwekeza kwenye sekta ya kilimo na hivyo kuongeza mnyororo wa thamani katika mazao ya kilimo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine amesema hilo ni azimio mojawapo lililofikiwa katika Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya OACPS uliofanyika jijini Brussels nchini Ubelgiji tarehe 8 na 9 Juni 2022 ambapo alimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula.
Amesema kuwa wadau wa kilimo kutoka Tanzania wanaotaka mikopo hiyo ya masharti nafuu watatakiwa kuomba fedha hizo kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na kuweza kushiriki kikamilifu katika mkakati huo wa kuongeza mnyororo wa thamani kwenye mazao ya kilimo
“ Mkutano umeazimia kuanzisha mkakati wa kuongeza mnyororo wa thamani katika mazao ya kilimo, na ili kufanikisha azimio hilo Jumuiya imetenga Euro milioni 157 ambazo zitatoka kama mikopo ya masharti nafuu kwa wakulima ndani ya jumuiya yetu ya OACPS” alisema Balozi Sokoine na kuongeza kuwa wadau wa kilimo kutoka Tanzania wataweza kuomba fedha hizo kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Ubelgiji.
Amesema kuwa Ubalozi ukikamilisha taratibu za uombaji na utoaji wa mikopo hiyo utatoa kwa walengwa ili wafanye maombi ya mikopo hiyo.
Akiongelea mazimio mengine ya mkutano huo Balozi Sokoine amesema kuwa ni kuidhinishwa kwa Tanzania katika nafasi ya Uenyekiti wa Kamati ya masuala ya Uvuvi kwa miaka miwili kuanzia 2022 hadi 2024 na hivyo kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Mawaziri wa masuala Uvuvi unaotarajiwa kufanyika nchini mwaka 2024.
“Hatua hii ni fursa kubwa kwa Tanzania katika kusimamia utekelezaji wa ajenda yake ya uchumi wa buluu na kukuza ushirikiano baina ya nchi za OACPS katika sekta ya uvuvi” alisema.
Amesema Mkutano huo umejadili changamoto zinazowakabili wafanyabiashara ndani ya jumuiya wakati wa kuingiza bidhaa katika soko la Ulaya na kuja na mikakati ya kutatua changamoto hizo kwa kufaya tathmini ya kina ili kuzielewa changamoto husika na kuanzisha mfumo wa utoaji tahadhari mapema kwa wafanyabiashara.
Amesema azimio lingine ni kuanzisha Jukwaa Maalum la Wafanyabiashara ndani ya Jumuiya kwa lengo la kuwakutanisha wafanyabiashara, kubadilishana uzoefu na kukuza mtandao wa masoko ya bidhaa na huduma na kuongeza kuwa Mkutano pia umeazimia kuunganisha nguvu ya Diaspora kwa kuanzisha jukwaa maalum la kuwezesha Diaspora kukaa pamoja na kubadilishana uzoefu kwenye masuala mbalimbali ikiwemo fursa za uwekezaji ndani ya Jumuiya na kutoa maoni na kufanyiwa kazi.