Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Alhajj Juma Killimbah akizungumza kwenye hafla hiyo. |
Meneja wa Benki ya NBC Mkoa wa Singida, Asia Chembaga akizungumza . |
Na Dotto Mwaibale, Singida
BENKI ya Taifa ya Biashara Tanzania (NBC) imetoa Sh. 50 Milioni kwa ajili
ya kuisaidia ujenzi wa kiwanja cha kisasa kitakacho jengwa eneo la Mtipa nje
kidogo ya Manispaa ya Singida.
Kiwanja hicho kitakuwa kikimilikiwa na Timu ya Singida Big Star ambayo imeingia
msimu huu kushiriki mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kupanda
daraja.
Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea fedha hizo Mkuu wa Mkoa wa Singida
Dk.Binilith Mahenge ameishukuru benki hiyo kwa kusikia kilio cha muda mrefu cha
wadau wa michezo mkoani hapa na kukubali kuchangia kiasi hicho cha fedha.
“Maombi ya wadau wa mkoa, chama na wawakilishi wetu Bbenki ya NBC
wameyasikia na kuamua kutupatia kiasi hiki cha fedha hongereni sana NBC
tutahakikisha fedha hizi zinakwenda kufanya kazi iliyokusudiwa na si
vinginevyo” alisema Mahenge.
Mahenge alisema anatamani sana kuona sasa kuna kuwa na mechi za mfululizo
zikifanyika katika uwanja wa zamani na huo mpya ukikamilika ili wananchi wa Mkoa
wa Singida wafaidike kwa kupata burudani ya mechi mbalimbali.
Alisema kujengwa kwa viwanja vingi vya michezo kutafungua fursa kwa
wafanyabiashara wenye mahoteli na makundi mengine ya kupata fedha na hata kuhufanya
mji wa Singida kupanuka.
Dk. Mahenge alisema kukamilika kwa viwanja hivyo ambavyo vitajengwa eneo
hilo la Mtipa na pembeni mwa barabara ya
kutoka Singida kwenda Arusha vitapendezesha mji wa Singida na kuwa kimbilio la
wageni kwenda kupumzika kutokana hewa nzuri inayopatika mkoani humo.
Aidha Dk.Mahenge aliendelea kuipongeza benki hiyo kwa kujitoa kuisadia
Serikali na kueleza kuwa hata alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma alishuhudia
benki hiyo ikitoa msaada mkubwa na hata magari na alitumia nafasi hiyo
kuwaeleza kuwa Serikali mkoani hapa itaendelea kushirikiana nayo ambapo alitoa
wito kwa timu ya Singida Big Star itakayosimamia ujenzi wa kiwanja hicho
kuhakikisha kinajengwa kwa viwango kutokana na eneo kilipo kiwanja hicho kuhitaji
utaalamu na kuwa wahandisi wa mkoa na Mkuu wa Wilaya ya Singida ambaye ni
Mhandisi wataipitia michoro ili ujenzi huo uwe sawasawa.
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya mkurugenzi mkuu wa benki hiyo, Daudi
Raymond ambaye ni Mkurugenzi wa Masoko wa benki hiyo alisema wamekuwa wakitoa
huduma za kibenki mkoani hapa kwa miongo
mingi na kuwa wanajivunia kuwa wa kwanza.
Alisema benki hiyo ni mdau mkubwa wa maendeleo hapa nchini kama kauli mbiu yao inavyosema daima karibu
nawe tunathaamini umuhimu wa kuwa karibu na wateja wetu, wadau na jamii kwa
ujumla.
Alisema sera yao ya kurudisha faida wanayoipata kwa jamii imejikita katika
sehemu kuu tatu, elimu, afya ya mama na mtoto pamoja na maendeleo ya jamii
ikiwemo michezo mbalimbali.
Raymond alisema katika kipindi cha mwaka uliopita benki hiyo iliweza
kusaidia zaidi ya Sh.Bilioni 1 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kijamii na
kiasi hicho ni nje ya Sh.9 Bilioni waliyotoa kwa ajili ya kudhamini Ligi Kuu ya
Tanzania Bara kwa kipindi cha misimu mitatu.
Alisema wanajivunia kushiriki maendeleo ya soka hapa nchini na kuwa wataendelea kutoa michango kwa ajili
ya kuboresha miundombinu ya michezo kama soka, riadha, gofu na mingine mingi na
kuwa benki hiyo inaamini kuwa michezo ni afya na ajira hivyo wanafuraha kubwa
kukabidhi kiasi hicho cha fedha ambazo zimelenga kuboresha uwanja wa michezo na
matumaini yao kuwa mchango huo utasaidia kuinua na kuibua vipaji vya michezo mkoani Singida.
Raymond alitumia nafasi hiyo kuwakaribisha wakazi wa Singida kwenye tukio
mashuhuri la Dodoma NBC Marathoni ambalo Kitaifa litafanyika Julai 31, 2022
kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma lenye lengo ya kukusanya fedha kwa ajili
ya kongamano la saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake ambapo wanashirikiana
na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida Alhajj Juma Killimbah alisema ujenzi wa viwanja hivyo ni utekelezaji wa Ilani ya chama hicho katika kudumisha michezo hapa nchini kwani chama hicho kilianza zamani kuvijenga na ndio maana vipo katika mikoa yote.