Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Mwanza Edwin Soko akizungumza kwenye mkutano wa majadiliano ya mwenendo wa taaluma ya habari Nchini
Meneja wa Mamlaka ya mawasiliano TCRA Kanda ya ziwa Mhandisi Francis Mihayo akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano wa majadiliano ya mwenendo wa taaluma ya habari ulioandaliwa na chama cha waandishi wa habari MPC na Internews
Waandishi wa habari pamoja na viongozi mbalimbali wakiwa kwenye picha ya pamoja
………………………………………….
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Mwanza (MPC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Internews imefanya mkutano wa majadiliano ya mwenendo wa taaluma ya habari.
Mkutano huo umefanyika leo Juni 9,2022 katika ukumbi wa Gold crest uliopo Jijini Mwanza.
Akizungumza wakati wa kufungua mkutano huo Meneja wa Mamlaka ya mawasiliano (TCRA) Kanda ya ziwa Mhandisi Francis Mihayo, amesema waandishi wa habari wajikite katika kuandika habari zenye tija kwani kwakufanya hivyo itasaidia kuwaepusha na migogoro katika Jamii na Taifa kwa ujumla.
Mihayo ametoa wito kwa waandishi wa habari kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa kuielimisha jamii, kuihabarisha kupitia habari mbalimbali wanazozifanya.
Kwaupande wake Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Mwanza (MPC) Edwin Soko, amesema miongoni mwa malengo ya mkutano huo ni kuhakikisha waandishi wa habari wanazijua sheria za habari ili waweze kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa.
Soko ameeleza kuwa wamekuwa wakishirikiana na Taasisi ya Internews katika kuandaa mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari na kuwakumbusha kufanya kazi kwakufuata sheria na taratibu za Nchi.