Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi (kushoto),akipokea msaada wa mdawaati 355 kati ya 455, viti 108 na meza 18 kutoka kwa Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation (TD &FC) Alhaji Sibtain Meghjee (kulia), wa kwanza kushoto ni Diwani wa Nyamagana (CCM) Bhiku Kotecha amsaada uliogharimu sh. milioni 65.
***********************
NA BALTAZAR MASHAKA, Nyamagana
TAASISI ya The Desk & Chair Foundation (TD & CF) Tawi la Tanzania imekabidhi msaada wa madawati 455,viti 18 na meza ili kutatua changamoto ya upungufu wa madawati katika shule za sekondari za umma wilayani humu.
Msaada huo wa madawati kwa ajili ya wanafunzi,viti na meza za walimu wenye thamani ya sh.milioni 65 umetolewa na wadau mbalimbali wakishirikiana na The Desk & Chair Foundation na kukabidhiwa juzi kwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,Amina Makilagi.
Meghjee alisema taasisi hiyo imekuwa bega kwa bega na serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya jamii inayolenga kuinua na kuboresha maisha ya wananchi wenye changamoto ikishirkiana pia na taasisi mbalimbali zenye malengo yanayofanana pamoja na serikali ili kuleta maendeleo.
“Ninayo furaha kukambia kuwa madawati hayo yote yamefadhiliwa na Waislamu wa madhahebu ya Shia Ithna Asheria wengi wao wana asili ya Mkoa wa Mwanza,nakuomba uridhie kupokea mdawati 355 ya shule za sekondari za serikali,mengine 208 tutakabidhi taasisi ya Bilal Muslim Mission of Tanzania kwa shule za chekechea na 100 kwa maelekezo ya wafadhili,”alisema.
Meghjee alieleza kuwa taasisi hiyo iliyoanzishwa nchini Uingereza na wazaliwa wa Mwanza kutoka familia yao kisha kusajiliwa nchini, wanatekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa matundu 20 ya vyoo Kilimani Sekondari ya Ilemela.
Pia mingine ni kujenga miundombinu na kuchimba kisima kirefu cha maji katika Gereza Kuu la Butimba mkoani Mwanza na uboreshaji wa kisima kirefu cha zahanati moja iliyo mkoani Simiyu.
Kwa mujibu wa Meghjee,wamekamilisha mradi mkubwa wa kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria na kuyasambaza katika Hospitali ya Bukumbi Mission,mradi wa maji na ufugaji wa ng’ombe na mbuzi katika Kambi ya Wazee Bukumbi na mradi wa magodoro 1000 Gereza la Butimba.
Aidha wametoa vyerehani 200 kwa wajasiriamali wanawake,mradi wa kutibu macho (mtoto wa jicho)unaendelea katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando ambapo watagharamia watu 100 kufanyiwa upasuaji wa macho na kipindi cha Ramadhani walifadhili vyakula anuwai kwa familia 4500 zisizojiweza katikaa mikoa tisa ya Kanda ya Ziwa,Kati na Magharibi.
Akipokea madawati hayo, Makilagi aliwashukuru wafadhili kwa kuguswa na changamoto ya watoto kukaa chini darasani na kwamba mbali na changamoto ya vyumba vya madarasa,uhaba wa walimu katika shule za msingi na sekondari, madawati nayo yameongeza changamoto katika sekta ya elimu.
Alisema changamoto hiyo iliwalazimu wazazi kuchangia madawati katika shule za msingi na sekondari ili kuunga jitihada za serikali na kuwawesha watoto kujifunza katika mazingira bora.
Makilagi alisema madawati imekuwa changamoto kubwa kwa shule nyingi za serikali kutokana na ongezeko la wanafunzi waliojiunga na kidato cha kwanza kuwa kubwa kwa hivi karibuni licha ya Rais Samia Suluhu Hassan kujenga vyumba 15,000 nchi nzima yakiwa na samani zake(madawati).